Wakongo wafanya mandamano makubwa dhidi ya waasi wa M23 mjini Bukavu
(last modified Fri, 04 Nov 2022 11:25:55 GMT )
Nov 04, 2022 11:25 UTC
  • Wakongo wafanya mandamano makubwa dhidi ya waasi wa M23 mjini Bukavu

Wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wenye hasira wamechoma moto bendera ya Umoja wa Ulaya katika mji wa Bukavu mashariki mwa nchi hiyo, huku mamia ya wakiandamana dhidi ya waasi wa M23. Wananchi hao wameeleza kutoridhishwa kwao na uingiliaji wa mataifa makubwa kama vile Marekani, Uingereza na Ufaransa katika masuala ya ndani ya nchi yao.

Waandamanaji hao pia wamezituhumu nchi za Rwanda na Uganda kwamba zinaliunga mkono na kulisaidia kundi la waasi wa M23 kwa kufadhiliwa na madola makubwa kama Marekani na Uingereza. 

Wakati huo huo Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amewatoea wito vijana nchini humo kujikusanya kimakundi na kujiweka katika hali ya tahadhari kwa ajili ya kukabiliana na uasi wa kundi la M23. Amesema kundi hilo linanufaika na uungaji mkono wa serikali ya Rwanda. 

Akihutubia wananchi kwa njia ya televisheni, Rais Felix Tshisekedi ameishutumu Rwanda kuwa ina lengo la kujitanua na kwamba nia yake kuu ni kupora madini ya Kongo. Amesema, Rwanda inachukua hatua za kuyumbisha maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kukidhi malengo yake ya uhalifu. 

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo 

Kwa miongo mitatu sasa maeneo ya mashariki mwa Kongo yametumbukia katika hali ya mchafukoge inayosababishwa na makundi yanayobebe silaha; aghalabu yao yakiwa yale yaliyoshiriki katika vita vilivyoligubika eneo hilo baada ya mauaji ya kimbari ya Rwanda ya 1994. 

Hali ya mvutano imepamba moto kati ya serikali za Kinshasa na Kigali tangu mwishoni mwa mwaka jana wakati kundi la waasi wa (M23) lilipoibuka tena.

Tags