Watu 20 wauawa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika mapigano ya kikabilla
(last modified Thu, 10 Nov 2022 04:14:23 GMT )
Nov 10, 2022 04:14 UTC
  • Watu 20 wauawa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika mapigano ya kikabilla

Kwa akali watu 20 wameuawa wiki hii katika shambulio lililotokea magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Hayo yameelezwa na maafisa wa eneo hilo ambapo ghasia za kikabila zimekuwa zikiendelea kwa miezi kadhaa sasa.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, mauaji hayo yametokea katika kijiji cha Boku, huko Kwamouth katika jimbo la Mai-Ndombe, ambalo limekuwa likishuhudia mapigano kati ya watu wa Yaka na Teke tangu Juni mwaka huu.

Nkete Mboma Butu, mwakilishi wa asasi ya kiraia huko Kwamouth ameziambia duru za habari kwamba, siku ya Jumatatu watu wasiojulikana wakiwa na bunduki walishambulia kijiji cha Teke.

Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limekuwa likishuhudia ukosefu wa amani na usalama kwa miaka kadhaa sasa kutokana na kuweko harakati za makundi ya wanamgambo ambayo yamekuwa yakifanya mauaji katika maeneo hayo.

Maelfu ya raia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemorasia ya Congo wamelazimika kuyakimbia makazi yao wakihofia usalama wa maisha yao

 

Jeshi la DRC na vikosi vya kusimamia vya Umoja wa Mataifa MONUSCO vimekuwa vikikosolewa kutokana na kushindwa kulinda usalama wa raia katika maeneo hayo.

Hivi karibuni wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo waliokuwa na ghadhabu walichoma moto magari ya askari walinda amani wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaojulikana kwa jina la MONUSCO, wakisisitiza kuwa kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa kimeshindwa kukabiliana na harakati na mashambulizi ya kundi la waasi la M23 na kutoa mwito wa kuondoka nchini humo haraka iwezekanavyo, kwani uwepo wake haujasaidia chochote katika kurejesha usalama na uthabiti nchini humo.

Tags