Maandamano yaendelea Sudan kulalamikia uingiliaji wa nchi ajinabi
Maelfu ya watu wameandamana Sudan wakitaka kukomeshwa uingiliaji wa nchi ajinabi katika masuala ya ndani ya nchi hiyo.
Sudan inahitaji msaada wa jamii ya kimataifa na hasa Umoja wa Mataifa ili kuiepusha nchi hiyo na uwezekano wa kutumbukia katika vita vya ndani. Hii ni katika hali ambayo, maafisa na wachambuzi wa mambo huko Sudan wametahadharisha kuwa taasisi za kimataifa zinatumia vibaya hali ya mambo ya ndani ya nchi hiyo kama kisingizio cha kuingilia masuala ya ndani ya Sudan.
Kundi kwa jina la "Sudan Call Initiative Group" na harakati nyingine za Kiislamu za nchi hiyo jana ziliandamana mbele ya ofisi ya Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa huko Khartoum na kusisitiza kuhitimishwa uingiliaji kati wa pande za kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo.
Baadhi ya waandamanaji wamesisitiza kuwa, wananchi wa Sudan wanaweza kutatua matatizo yao wenyewe bila ya uingiliaji kati wa wawakilishi na balozi zozote za nchi ajinabi. Waandamanaji walikuwa wamebeba mabango yenye maandishi "hatutaki uingiliaji wa nchi ajinabi, tunapinga rasimu mpya ya katiba na mapatano ya kisiasa."
Sudan, ambayo ni miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani, imekumbwa na mzozo wa kisiasa tangu mwaka jana 2021 kufuatia mapinduzi ya kijeshi.