Maporomoko ya ardhi yaua watu 14 mazishini nchini Cameroon
(last modified Mon, 28 Nov 2022 03:38:43 GMT )
Nov 28, 2022 03:38 UTC
  • Maporomoko ya ardhi yaua watu 14 mazishini nchini Cameroon

Watu wasiopungua 14 wamepoteza maisha kufuatia maporomoko ya ardhi yaliyotokea jana Jumapili nchini Cameroon.

Shirika la Utangazaji la Cameroon (CRTV) limeripoti kuwa, mkasa huo ulitokea jana, wakati makumi ya watu walikuwa wamekusanyika katika shughuli ya kuwazika jamaa zao katika eneo la Damas karibu na mji mkuu Yaoundé.

Gavana wa eneo la kati la Cameroon, Naseri Paul Bea aliwasili katika eneo la tukio kutathmini hali ya mambo, huku shughuli za kuwaokoa waliofukiwa kwenye vifusi zikiendelea.

CRTV imechapisha kwenye ukurasa wake wa Twitter picha zinazoonesha timu za waokoaji wakiendelea kusaka miili ya wahanga na kujaribu kuwaokoa watu waliofukiwa kwenye vifusi na udongo.

Ramani ya Cameroon

Watu wamesambaza kwenye mtandao wa Twitter video na picha za maafa na uharibifu uliotokea kwenye janga hilo la kimaumbile nchini Cameroon.

Yaoundé ni moja ya miji ya Afrika yenye miinuko na milima mingi. Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha zimesababisha mafuriko na maporomoko ya udongo katika pembe mbalimbali za nchi hiyo.