Malengo ya safari ya as-Sudani mjini Tehran
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i91166-malengo_ya_safari_ya_as_sudani_mjini_tehran
Mohammad Shia as-Sudani, Waziri Mkuu wa Iraq, aliwasili mjini Tehran Jumanne asubuhi kwa ziara ya siku mbili, na baada ya kukutana na mwenyeji wake Rais Ebrahim Raisi wa Iran, pia alikutana na kuzungumza na Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
(last modified 2024-06-10T09:25:34+00:00 )
Dec 01, 2022 04:03 UTC
  • Malengo ya safari ya as-Sudani mjini Tehran

Mohammad Shia as-Sudani, Waziri Mkuu wa Iraq, aliwasili mjini Tehran Jumanne asubuhi kwa ziara ya siku mbili, na baada ya kukutana na mwenyeji wake Rais Ebrahim Raisi wa Iran, pia alikutana na kuzungumza na Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Hii ni safari ya tatu ya kigeni ya Shia as-Sudani baada ya kuchaguliwa kuwa waziri mkuu wa Iraq. Safari yake ya kwanza ilifanyika huko Jordan na ya pili nchini Kuwait. Inasemekana kuwa Shia as-Sudani hivi karibuni pia atafanya safari huko Saudi Arabia na Uturuki. Safari hizi za nje zinaonyesha mwelekeo wa Waziri Mkuu mpya wa Iraq katika kupanua uhusiano na kutatua mizozo na nchi jirani.

Kuchaguliwa Iran kuwa miongoni mwa maeneo ya kwanza ya safari za nje za Waziri Mkuu mpya wa Iraq kunaonyesha kuwa, kwa upande mmoja anataka kupanua na kuimarisha uhusiano na Iran, na kwa upande mwingine Tehran pia imeazimia kupanua uhusiano wake na Baghdad. Ni wazi kuwa kuimarisha mashirikiano ya kiuchumi ni moja ya malengo ya safari ya Waziri Mkuu wa Iraq mjini Tehran. Mabadilishano ya kibiashara na kiuchumi kati ya Iran na Iraq kwa sasa ni ya takriban dola bilioni 12 kwa mwaka, ambapo mpango wa serikali ya 13 ya Tehran ni kuongeza kiwango hicho hadi kufikia dola bilioni 20.

Kuhusiana na suala hilo, Rais Seyyed Ebrahim Raisi katika kikao chake na Mohammad Shia as-Sudani Waziri Mkuu wa Iraq, ameeleza kuridhishwa kwake na uthabiti wa kisiasa na uundwaji wa serikali mpya ya Iraq na kusema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima inakaribisha na kuunga mkono taifa moja na serikali yenye nguvu nchini Iraq.

Shia as-Sudani pia alikutana na kuzungumza na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Akisisitiza azma ya Iran kupanua ushirikiano na kuboresha kiwango cha uhusiano wake na Iraq katika nyuga za kiuchumi, kibiashara, kisiasa, kiutamaduni na kiusalama, Rais Raisi ameongeza kuwa: Iran inataka kuendeleza mabadilishano na Iraq katika nyanja mbalimbali za kibiashara na pia nishati, na kufanyika mikutano ya mara kwa mara ya Tume ya Ushirikiano ya nchi mbili kunaweza kuwa na nafasi muhimu katika kufikiwa lengo hilo.

Ziara ya hivi sasa ya Shia al-Sudani mjini Tehran pia ina muhimu mkubwa katika suala zima la kufuatilia matukio ya eneo la Kurdistan la Iraq. Kufuatia kuibuliwa machafuko nchini Iran, eneo la Kurdistan linalopakana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa maeneo ambayo maadui wamekuwa wakiyatumia kwa ajili ya kuchochea machafuko humu nchini. Kwa mujibu wa taarifa kadhaa zilizotolewa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC, magaidi wa makundi ya Komaleh, Demokrat, Pejak, n.k wamekuwa yakilitumia eneo hilo la Iraq kuendeshea shughuli zao za kigaidi na kusababisha machafuko nchini Iran.

Kwa kuzingatia hayo, IRGC imefanya mashambulizi kadhaa dhidi ya magaidi hao walioweka kambi zao kaskazini mwa Iraq, na wakati huo huo kuitaka serikali ya Iraq na ya kieneo ya Erbil kuhakikisha kuwa usalama wa mpaka unadumishwa siku zote. Kwa hivyo, moja ya mambo muhimu yaliyofuatiliwa katika safari ya Shia ya as-Sudan nchini Iran ni kutaka kuimarishwa usimamizi wa serikali kuu ya Iraq katika eneo la Kurdistan na kuzuiwa maigaidi kujipenyeza na kuingia katika ardhi ya Iran kwa lengo la kufanya uharibifu na kuchochea machafuko nchini.

Kufuatilia mazungumzo ya Iran na Saudi Arabia ni lengo jingine la safari ya as-Sudani mjini Tehran. Hadi sasa, duru 5 za mazungumzo kati ya nchi hizi zimefanyika kwa upatanishi wa Baghdad. Serikali hii mpya ya Iraq pia inasisitiza juu ya kuendeleza mazungumzo kati ya Tehran na Riyadh, na inaonekana kwamba suala hilo limewasilishwa kwa viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika ziara hii ya Shia as-Sudani.

As-Sudani (kushoto) pia alionana na kuzungumza na Mohammad Bagher Ghalibaf, Spika wa Bunge la Iran

Jambo la mwisho ni kwamba inaonekana kuwa katika serikali mpya ya Iraq ambayo pia inaungwa mkono na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, uhusiano kati ya nchi hizi mbili utaimarika zaidi kuliko huko nyuma. Kuhusiana na hilo, Mohammad Shia as-Sudani, Waziri Mkuu wa Iraq, katika kikao na mwenyeji wake Rais Ebrahim Raisi, sambamba na kueleza kufurahishwa kwake na safari yake mjini Tehran mwezi mmoja baada ya kuundwa serikali mpya ya Baghdad, amesema: Iran ina nafasi bora na nzuri zaidi katika mahusiano na siasa za nje za Iraq, na kwa bahati nzuri uhusiano wa nchi mbili hizi unaendelea kupanuka kwa namna inayofaa na ya kuridhisha.