Jeshi la Kongo lawatuhumu waasi wa M23 kwa kuuwa raia 50
(last modified Fri, 02 Dec 2022 11:05:09 GMT )
Dec 02, 2022 11:05 UTC
  • Jeshi la Kongo lawatuhumu waasi wa M23 kwa kuuwa raia 50

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limelituhumu kundi la waasi la M23 na waitifaki wake kwamba wawaua raia 50 katika mji wa Kishishe mashariki mwa nchi hiyo.

Jeshi la Kongo limeeleza katika taarifa yake kuwa mauaji hayo yalijiri Jumanne wiki hii. Wakati huo huo jeshi hilo limewatuhumu waasi wa M23 kuwa wamekiuka usitishaji vita wa siku 5 mashariki mwa nchi hiyo. 

Makumi ya maelfu ya watu wamelazimika kuhama makazi yao kufuatia kuzuka mapigano mwezi uliopita kati ya jeshi la Kongo na waasi wa M23 mashariki mwa nchi hiyo. 

Jenerali Sylvain Ekenge wa jeshi la Kongo ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, waasi wa M23 wamekuwa wakitekeleza mauaji na kwamba ya karibuni zaidi ni yale waliyofanyika dhidi ya raia 50 waliouliwa kinyama katika mji wa Kishishe Jumanne wiki hii katika kijiji kilichoko umbali wa kilomita zisizopungua 70 kaskazini mwa mji wa Goma. 

Waasi wa kundi la M23 

Jenerali Ekenge amedai kuwa vikosi vya jeshi la Kongo vimeheshimu usitishaji vita uliotangzwa na kwamba waasi wa M23 wameshambulia ngome za vikosi vya serikali. Huku hayo yakiripotiwa, Bertranda Bisimwa kiongozi wa waasi wa M23 amesema watajibu tuhuma hizo dhidi baadaye kupitia taarifa watakayoitoa. 

Umoja wa Mataifa na shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) wameeleza kuwa, zina taarifa kuhusu mauaji yaliyotekelezwa huko Kishishe katika jimbo la Kivu ya Kaskazini. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inaituhumu nchi jirani yake Rwanda kuwa inawaunga mkono waasi wa kundi la M23, tuhuma ambazo zimekanushwa na Kigali. 

Tags