Viongozi wa kidini wakutana mashariki mwa Kongo kujadili hali ya mambo
(last modified Sun, 04 Dec 2022 11:43:18 GMT )
Dec 04, 2022 11:43 UTC
  • Viongozi wa kidini wakutana mashariki mwa Kongo kujadili hali ya mambo

Viongozi wa kidini wamekutana katika mji wa Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufuatia machafuko yaliyosababisha vifo vya watu 50 mashariki mwa nchi hiyo.

Itakumbukwa kuwa, Alhamisi iliyopita jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo lililituhumu kundi la waasi la M23 kwa mauaji hayo na kukiuka mapatano ya kusitisha vita yaliyofikiwa hivi karibuni. Mchungaji Samuel Ngahiembako Mwenyekiti wa Kanisa kwa jina Church of Christ in Congo ameeleza kuwa: Wamejitolea kwa mpango huo wa dini mbalimbali kwa ajili ya kurejesha amani huko Kivu Kaskazini na kuziunga mkono mamlaka husika jimboni humo katika juhudi zao za kurejesha amani na kuishi pamoja kwa maelewano. Aidha wametoa  wito kwa wananchi wote kushiriki katika juhudi za kurejesha amani huko Kongo.

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo juzi ametangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kufuatia machafuko yaliyojiri katika mji wa Kishishe mashariki mwa Kongo Jumanne iliyopita. Jeshi la Kongo limewatuhumu waasi wa M23 na waitifaki wao kwa kuhusika na mauaji hayo ya raia 50 katika mji huo.

Waasi wa kundi la M23 

Mkazi wa Goma kwa jina la Amani Fundiko amenukuliwa akisema: "Nimejawa na hofu kwa sababu hatuna amani wala furaha. Wapiganaji wetu wanauliwa huko Rutshuru, Runyonyi, Rugari na kwingineko. Tunataraji kuwa, Rais atachukua maamuzi ili kudhibiti hali ya mambo na kuona kuwa wanafanikiwa kusitisha uasi wa kundi la M23 katika barabara ya kutoka Goma kuelekea Rutshuru." 

Tags