Tigray yaunganishwa tena kwenye gridi ya umeme ya taifa
Makao makuu ya eneo la Tigray, Mekele, kwa mara nyingine tena yameunganishwa kwenye gridi ya umeme ya taifa baada ya kukosa umeme kwa zaidi ya mwaka moja kutokana na vita vilivyoliathiri eneo hilo la kaskazini mwa Ethiopia. Hayo yameelezwa na Kampuni ya Taifa ya Umeme ya nchi hiyo.
Ethiopia imetangaza kurejesha huduma ya umeme katika eneo la Tigray ikiwa imepita mwezi mmoja baada ya kusaini makubaliano ya amani tarehe 2 mwezi uliopita wa Novemba kati ya serikali ya Addis Ababa na waasi wa Tigray wa TPLF. Makubaliano hayo yamesainiwa kwa lengo la kuhitimisha mzozo wa miaka kadhaa katika eneo hilo.
Kampuni ya taifa ya Umeme ya Ethiopia imesema kuwa, njia ya usambazaji umeme katika eneo la Tigray zimeunganishwa kwenye gridi ya umeme ya taifa baada ya kukamilika matengenezo.
Tigray, eneo la kaskazini mwa Ethiopia ambalo lina jamii ya watu milioni sita, lilinyimwa huduma nyingi za kimsingi kama umeme, huduma ya mawasiliano ya simu, benki, mafuta, n.k. kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa tangu kuanza mapigano kati ya serikali Ethiopia chini ya uongozi wa Waziri Mkuu Abbiy Ahmed, na waasi wa harakati ya Tigray People's Liberation Front (TPLF).
Mapigano yalianza huko Tigray mwezi Novemba mwaka 2020 wakati Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, alipotuma vikosi vya jeshi kuwatia nguvuni viongozi wa eneo hilo ambao wamekuwa wakiitatiza serikali yake kwa muda huku akiwatuhumu kufanya mashambulizi dhidi ya kambi za jeshi la Ethiopia.