Zambia: Magendo ya binadamu yanatishia uhuru wa kusafiri Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i91456-zambia_magendo_ya_binadamu_yanatishia_uhuru_wa_kusafiri_afrika
Rais Hakainde Hichilema wa Zambia amesema magendo ya binadamu linasalia kuwa tishio kuu la uhuru wa kutembea na kusafiri kwa watu wa nchi za Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 08, 2022 07:48 UTC
  • Zambia: Magendo ya binadamu yanatishia uhuru wa kusafiri Afrika

Rais Hakainde Hichilema wa Zambia amesema magendo ya binadamu linasalia kuwa tishio kuu la uhuru wa kutembea na kusafiri kwa watu wa nchi za Afrika.

Hichilema amesema hayo wakati wa uzinduzi wa mradi wa kujenga kituo cha Mwami/Mchinji katika mpaka wa nchi hiyo na Malawi; utakaogharimu dola milioni 7.5 za Marekani.

Amesema kituo hicho cha mpakani kitatumia teknolojia ya kisasa ili kukabiliana ipasavyo na tatizo hilo la magendo ya binadamu, sambamba na kuwepesisha ufanyaji wa biashara kati ya nchi hiyo na majirani zake.

Zambia ni kituo kikuu cha magendo ya binadamu miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC). 

Akthari ya wanaotumbukia kwenye biashara hiyo haramu ni wahamiaji kutoka kanda ya Afrika Mashariki, wanaorubuniwa kwenda Afrika Kusini na Namibia eti kwa ajili ya fursa za ajira.

Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera ambaye pia alishiriki katika uzinduzi wa ujenzi wa kituo hicho cha mpakani na nchi jirani ya Zambia amesema kituo hicho kitawepesisha usafirishaji wa watu wa bidhaa na hivyo kupiga jeki biashara baina ya nchi mbili hizo.

Hivi karibuni, maiti kadhaa za wahajiri haramu raia wa Ethiopia zilipatikana nchini Malawi, huku mtoto wa kambo wa rais wa zamani wa nchi hiyo akikamatwa akihusishwa na sakata hilo.

Idadi kubwa ya wahamiaji haramu wa Kiafrika haswa kutoka nchi za Malawi, Zambia, Msumbiji na Tanzania wamekamatwa katika siku za hivi karibuni katika nchi mbili hizo wanachama wa SADC.