UN yaeleza wasiwasi wake kuhusu mauaji ya raia Congo DR
(last modified Sat, 10 Dec 2022 08:13:20 GMT )
Dec 10, 2022 08:13 UTC
  • UN yaeleza wasiwasi wake kuhusu mauaji ya raia Congo DR

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema mauaji ya raia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yanatia wasiwasi.

Volker Turk amesema kuwa, "Kuna haja kubwa ya kukomesha mapigano yanayoendelea katika mikoa mbalimbali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, hasa katika mkoa wa Kivu Kaskazini."

Afisa huyu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa: Daima raia ndio wanaoteseka kutokana na mapigano na ukosefu wa uhuru wa kidemokrasia.

Uchunguzi uliofanywa na ofisi ya uwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umegundua kuwa takriban raia 131 waliuawa katika mashambulio yaliyofanywa Novemba 29 na 30 na kundi la waasi la M23.

Hata hivyo Jumatatu iliyopita, maafisa wa serikali ya Congo walitangaza kuwa idadi ya waliouawa katika kijiji cha Kishishe katika jimbo la Kivu Kaskazini ni karibu watu 300.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC Monusco umesema kuwa, wanawake wapatao 22 na wasichana 5 walibakwa na wanamgambo wa kundi la M23.

Mashariki mwa Congo

Ripoti hiyo ya wachunguzi wa Umoja wa Mataifa imefafanua kuwa hujuma hizo zimefanywa kama sehemu ya kampeni ya mauaji, ubakaji, utekaji nyara na uporaji dhidi ya vijiji viwili katika eneo la Rutshuru ikiwa ni kulipiza kisasi, kufuatia mapigano kati ya M23 na makundi mengine ya wabeba silaha pamoja na jeshi la serikali FDLR.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa idadi halisi ya waliouawa inaweza kuwa kubwa zaidi.

Tags