Waasi wa M23 wateka nyara raia 52 mashariki mwa DRC
(last modified Sun, 25 Dec 2022 10:38:46 GMT )
Dec 25, 2022 10:38 UTC
  • Waasi wa M23 wateka nyara raia 52 mashariki mwa DRC

Waasi wa M23 wameripotiwa kuwateka nyara raia 52 katika kijiji cha Rusekera kilichoko katika jimbo la Kivu Kaskazini huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Luteni Andrew Ruhaka, afisa mwandamizi wa jeshi la DRC alisema hayo jana Jumamosi na kuongeza kuwa, waasi hao walivamia kijiji hicho kilichoko katika eneo la Rutshuru na kuwafanya wakazi wake waanze kukimbia huku na kule. Ruhaka ameongeza kuwa, "Watu 52 walikusanywa na kuingizwa kwa nguvu kwenye lori, kisha wakepelekwa kusikojulikana." 

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa jeshi la Kongo DR amebainisha kuwa, waasi wa M23 wanaonekana kutaka kuwasajili wapiganaji wapya, baada ya kupokea vipigo kutoka kwa askari wa DRC na Uganda katika operesheni zilizoanza tokea Disemba 2021.

Utekeji huo wa raia unaripotiwa katika hali ambayo, jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki lililoko Kongo DR karibuni hivi lilitangaza kuwa, waasi hao wa M23 wameanza kuondoka katika maeneo waliyoyateka na kuyakalia kwa mabavu ya mashariki mwa nchi hiyo.

Waasi wa M23

Mapema jana Ijumaa, waasi hao wa M23 walitangaza kuanza kuondoka katika eneo la Kibumba lililoko umbali wa kilomita 20 kutoka Goma, makao makuu ya jimbo la Kivu Kaskazini. Hata hivyo jeshi la DRC limelitaja kuwa 'hadaa' tangazo la M23 la kuanza kuondoka mashariki mwa nchi hiyo.

Serikali ya Kongo imeishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23. Kigali imekanusha madai hayo. Hata hivyo wataalamu wa Umoja wa Mataifa karibuni walisema wana ushahidi wenye mashiko, unaoonesha kuwa askari wa serikali ya Rwanda wapo mashariki mwa DRC, ama kwa ajili ya kuwaunga mkono waasi wa M23, au kufanya operesheni za kijeshi dhidi ya makundi mengine ya waasi katika eneo hilo.

 

Tags