Sudan yautaka Umoja wa Mataifa uiondolee haraka vikwazo vya silaha
Sudan inalitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liifutie nchi hiyo vikwazo vya silaha haraka iwezekanavyo, vilivyowekwa mwaka 2005 kutokana na vita katika eneo la Darfur, magharibi mwa nchi.
Balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa, Al-Harith Idriss Mohamed, kupitia barua yake kwa Baraza la Usalama iliyosambazwa jana Ijumaa, amesema vikwazo hivyo havina tena itibari na umuhimu, kwani haviendani na hali halisi ya hivi sasa katika eneo la Darfur.
Mwandiplomasia huyo wa Sudan amesisitiza kuwa, "Darfur, kwa asilimia kubwa, hivi sasa imeondokana na hali ya vita, sambamba na changamoto za huko nyuma za kisiasa na kiusalama."
Balozi huyo wa Sudan katika Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa, serikali ya mpito ya kijeshi imejitolea kwa dhati kushughulikia matatizo ya kiusalama na kijamii yaliyosalia katika eneo hilo, yakiwemo mapigano ya kikabila ya mara kwa mara.
Agosti mwaka uliopita, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya jinai (ICC), Karim Khan alisema kuwa, Sudan imeahidi kutoa ushirikiano kamili katika uchunguzi wa uhalifu wa kivita na ukatili uliotekelezwa katika jimbo la Darfur chini ya uongozi wa rais aliyeondolewa madarakani Omar Hassan al-Bashir.
Eneo la Darfur mwaka 2003 lilikumbwa na mapigano ya umwagaji damu kati ya serikali ya wakati huo ya Sudan chini ya uongozi wa Rais aliyeondolewa madarakani al-Bashir, na wapinzani wa serikali.
Malaki ya watu waliuawa na mamilioni ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi katika mashambulizi hayo; na tokea wakati huo, eneo hilo limekuwa uwanja wa mapigano na umwagaji damu.