Mapigano kati ya jeshi la Kongo na wanamgambo mashariki mwa nchi
Duru za kijeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimearifu kuhusu kujiri mapigano kati ya askari jeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya makundi yenye silaha mashariki mwa nchi.
Duru za kijeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimeripoti kuwa jeshi la Kongo na walinda amani wa Umoja wa Mataifa wamepambana na makundi yenye silaha katika eneo la Buleusa mashariki mwa nchi hiyo. Duru hizo zimesisitiza kuwa mapigano hayo yamesabisha vifo vya wanamgambo sita na kujeruhi wengine kumi. Duru za kijeshi za Kongo zimeongeza kuwa wanamgambo wenye silaha ambao mwanzoni mwa wiki hii walituhumiwa kuchoma moto kambi moja ya wakimbizi katika eneo la Buleusa walikuwa ni kutoka katika kundi la waasi wa Kihutu wa Rwanda. Wakimbizi waliokuwa wakiishi kwenye kambi hiyo iliyochomwa moto hivi sasa wamepewa hifadhi karibu na kambi moja ya jeshi la Kongo. Maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yanakabiliwa na mizozo ya silaha, ukosefu wa amani na mapigano makali tangu miaka 20 iliyopita; hali ambayo inatajwa kusababishwa na makundi yenye silaha.