Wanachuo wa Sudan wapinga uhusiano wa kawaida na Israel
Wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini Sudan wamefanya maandamano katika mji mkuu Khartoum kupinga hatua ya utawala wa kijeshi wa nchi hiyo ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Sambamba na kutangaza mfungamano wao na wananchi madhulumu wa Palestina, wanachuo hao waliokusanyika nje ya Chuo Kikuu cha Khartoum jana jioni wamekosoa vikali hatua ya kiongozi wa kijeshi wa nchi hiyo, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ya kujikurubisha kwa utawala wa Kizayuni.
Ali Muhammad, mmoja wa wanafunzi hao walioandamana jana ametangaza wazi kwamba, kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel ni khiyana na usaliti si tu kwa Wapalestina, bali kwa uliwengu wote wa Kiarabu na Kiislamu.
Naye Alawiya al-Nayer, mwanachuo wa kike aliyeshiriki pia kwenye maandamano hayo jijini Khartoum amesema kuwa, hawatasitisha maandamano yao ya kuishinikiza serikali ya nchi hiyo ikate uhusiano na Wazayuni akisisitiza kuwa, uhusiano huo hauna maslahi yoyote kwa Wasudani.
Jumapili ya Februari 5 pia, wananchi wa Sudan waliandamana katika mji mkuu Khartoum kwa shabaha ya kupinga hatua ya utawala wa kijeshi nchini humo ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Waandamanaji hao sambamba na kulaani safari ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa utawala haramu wa Israel Eli Cohen aliyetembelea Sudan na kukutana na mkuu wa jeshi na kiongozi wa nchi hiyo, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, walisikika wakipiga nara dhidi ya Israel.
Oktoba mwaka 2020 Rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump alitangaza kuwa Sudan na Israel zimefikia mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida ikiwa na maana ya Sudan kujiunga na nchi zingine za Kiarabu na Kiislamu za Misri, Jordan, Imarati na Bahrain kuutambua rasmi utawala huo haramu unaoikalia kwa mabavu Palestina na Quds tukufu.