UNHCR: Dola bilioni 1.3 zinahitajika kusaidia wakimbizi wa Sudan Kusini
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, pamoja na mashirika 108 ya utoaji wa misaada ya kibinadamu wametoa ombi la dola bilioni 1.3 ili kusaidia wakimbizi kutoka Sudan Kusini na jamii zinazowahifadhi katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, Ethiopia, Kenya, Sudan na Uganda.
Msemaji wa UNHCR jijini Geneva, Uswisi, Shabia Mantoo amewaeleza waandishi wa habari kwamba ombi hilo la fedha linatolewa wakati mwelekeo wa uchumi katika ukanda mzima wa eneo hilo ukiwa mbaya wakati madhara ya muda mrefu ya janga la COVID-19 yakizidi kuibuka bila kusahau changamoto zitokanazo na vita ya Ukraine, ongezeko la bei za vyakula na ukosefu wa ajira.
Bi. Mantoo amesema, “nchi zilizowakaribisha kwa ukarimu wakimbizi kutoka Sudan Kusini zinabeba mzigo mkubwa wakati ambapo ufadhili nao unasuasua, ukame wa muda mrefu na uhaba mkubwa wa chakula ikiwemo makato ya mgao wa chakula kwa wakimbizi."
Wakati uzinduzi wa ombi hilo, UNHCR imesihi jamii ya kimataifa iongeze misada yake kwa wakimbizi ambao hawawezi kurejea nyumbani kutokana na hali ya usalama kuwa tete pamoja na kuweko kwa madhara ya janga la tabianchi.
Miaka minne ya mafuriko yasiyokwisha yameathiri vibaya theluthi mbili ya Sudan Kusini, yakiharibu makumi ya maelfu ya makazi ya watu, mashamba na mifugo.
Bi. Mantoo amesema usaidizi huu utakuwa muhimu ili kukidhi mahitaji ya haraka ya wakimbizi kwenye nchi walikokimbiliia hifadhi, mahitaji kama vile makazi, elimu, afya na msaada wa chakula.
Nchi tano ambazo ni kimbilio kwa wasaka hifadhi Afrika, yaani DRC, Ethiopia, Sudan, Ethiopia na Uganda zimepokea kiwango kidogo cha fedha.