Muungano wa Madaktari wa Sudan Kusini waitaka serikali kushughulikia mlipuko wa kipindupindu
(last modified Wed, 26 Mar 2025 07:48:35 GMT )
Mar 26, 2025 07:48 UTC
  • Muungano wa Madaktari wa Sudan Kusini waitaka serikali kushughulikia mlipuko wa kipindupindu

Muungano wa Madaktari wa Sudan Kusini (SSDU) umeitaka serikali kushughulikia mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu unaoongezeka nchini humo. Ugonjwa wa kipindupindu tayari umeenea katika majimbo kadhaa ya Sudan Kusini na hivyo kuyaweka hatarini maisha ya maelfu ya watu.

Idara za afya za Sudan Kusini zimetangaza kuwa hadi sasa watu 700 wameaga dunia kwa kipindupindu na wengine zaidi ya 40,800 wamethibitika kuugua maradhi hayo kote nchini tangu mwezi Oktoba mwaka jana ulipotangazwa mlilpuko huo kuiathiri Sudan Kusini. 

Luka Dut Katibu Mkuu wa Muungano wa Madaktari wa Sudan Kusini amesema kuwa afya ya jamii na afya ya umma ni jukumu la serikali na inapasa kuchukua hatua zote katika uwanja huo. 

Dut ameongeza kuwa serikali yoyote ina jukumu la kushughulikia afya ya watu wake na Wizara ya Afya inahitaji fedha ili kusambaza vifaa tiba na huduma za matibabu katika maeneo yaliyoathirika. 

"Hali ni mbaya na hatua za dharura zinapasa kuchukuliwa ili kuzuia maafa zaidi na watu kupoteza maisha," ameongeza Katibu Mkuu wa Muungano wa Madaktari wa Sudan Kusini. 

Muungano wa Madaktari wa Sudan Kusini (SSDU) umetoa taarifa ukisema kuwa mlipuko wa kipindupindu ulioikumba nchi hiyo si tu ni dharura ya afya bali ni mgogoro wa kibinadamu uliochochewa zaidi na upatikanaji duni wa maji safi, huduma chache za kiafya na mfumo wa afya unaolegalega.