UN yasimamisha ndege zake kuruka Kivu Kaskazini, DRC
(last modified Mon, 27 Feb 2023 10:39:16 GMT )
Feb 27, 2023 10:39 UTC
  • UN yasimamisha ndege zake kuruka Kivu Kaskazini, DRC

Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO) kimetangaza habari ya kusimamisha ndege zake kuruka katika anga ya mkoa wa Kivu Kaskazini, baada ya helikopta yake kushambuliwa katika eneo hilo Ijumaa iliyopita.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu na Shirika la Huduma za Dharura za Anga la Umoja wa Mataifa (UNHAS) na Msemaji wa Mpango wa Chakula Duniani wa umoja huo (WFP) katika mahojiano na shirika la habari la Reuters.

Claude Kalinga, Msemaji wa WFP nchini Kongo DR amesema ndege za MONUSCO hazitaruka kwa muda usiojulikana katika makao makuu ya mkoa wa Kivu Kaskazini, Goma na miji ya mashariki ya Beni na Bunia. 

Hii si mara ya kwanza kwa ndege ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO) kushambuliwa na magenge ya waasi nchini DRC.

Mapema mwezi huu wa Februari, shambulio jingine dhidi ya helikopta ya ujumbe wa MONUSCO, lilisababisha kifo cha mlinda amani mmoja wa UN kutoka Afrika Kusini na mwingine kujeruhiwa.

Wanajeshi wa MONUSCO nchini DRC

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres alilaani vikali hujuma hiyo na kusisitiza kuwa, shambulizi dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa linaweza kuwa uhalifu wa kimataifa kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Wanachama wa kundi la waasi la M23 wameendelea kuyumbisha usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, licha ya uwepo wa askari wa UN, wanajeshi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na vikosi vya usalama vya DRC.

 

Tags