Burkina Faso yatangaza 'kafyu' ili kuzima hujuma za kigaidi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i94780-burkina_faso_yatangaza_'kafyu'_ili_kuzima_hujuma_za_kigaidi
Burkina Faso imeyaweka maeneo ya Kaskazini na sehemu ya katikati ya Mashariki mwa nchi chini ya amri ya kutotoka nje nyakati za usiku, ili kupiga jeki juhudi za kupambana na harakati na mashambulizi ya makundi ya kigaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 06, 2023 03:26 UTC
  • Burkina Faso yatangaza 'kafyu' ili kuzima hujuma za kigaidi

Burkina Faso imeyaweka maeneo ya Kaskazini na sehemu ya katikati ya Mashariki mwa nchi chini ya amri ya kutotoka nje nyakati za usiku, ili kupiga jeki juhudi za kupambana na harakati na mashambulizi ya makundi ya kigaidi.

Shirika la habari la AFP liliripoti habari hiyo jana Jumapili, likinukuu taarifa ya Katibu Mkuu ya serikali ya jimbo la Kaskazini, Kouilga Albert Zongo.

Taarifa hiyo imesema, chini ya mpango wa kupambana na ugaidi, amri ya kutotoka nje kuanzia saa nne usiku hadi saa kumi na moja alfajiri ilianza kutekelezwa kuanzia Machi 3 na itaendelea hadi Machi 31.

Amri hiyo pia imepiga marufuku magari na pikipiki kuwepo barabarani ndani ya muda huo wa kafyu. Zongo amesema agizo hilo litasaidia kudhibiti harakati za makundi ya kigaidi katika eneo hilo lililoko katika mpaka wa Mali, kulikoanzia uasi mwaka 2015.

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Februari, kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) lilitangaza kuwa limehusika kwenye mauaji ya zaidi ya wanajeshi 70 na kujeruhi wengine kadhaa na kutekwa nyara watu watano wakati wa shambulizi la kushtukiza dhidi ya msafara wa kijeshi kaskazini mwa Burkina Faso.

Magaidi Burkina Faso

Maelfu ya watu wameuawa na wengine zaidi ya milioni mbili wamekimbia makazi yao tangu magaidi hao wakufurishaji waanze kuishambulia Burkina Faso kutokea nchi jirani ya Mali mnamo 2015.

Hujuma na mashambulio ndani ya ardhi ya Burkina Faso yamechochea kuzuka mapinduzi mawili mwaka jana yaliyofanywa na maafisa wa jeshi waliokasirishwa na kuongezeka idadi ya raia wanaouawa katika mashambulio hayo.