Waislamu Nigeria waadhimisha kumbukumbu ya mazazi ya Imam Mahdi (AF)
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i94872-waislamu_nigeria_waadhimisha_kumbukumbu_ya_mazazi_ya_imam_mahdi_(af)
Waislamu wa madhehebu ya Shia na wafuasi na wapenzi wa Ahlu Bait (AS) nchini Nigeria wamejiunga na wenzao kote duniani katika maadhimisho ya kukumbuka kuzaliwa Imam wa Zama, Mahdi (AF).
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 08, 2023 10:26 UTC
  • Waislamu Nigeria waadhimisha kumbukumbu ya mazazi ya Imam Mahdi (AF)

Waislamu wa madhehebu ya Shia na wafuasi na wapenzi wa Ahlu Bait (AS) nchini Nigeria wamejiunga na wenzao kote duniani katika maadhimisho ya kukumbuka kuzaliwa Imam wa Zama, Mahdi (AF).

Mjini Abuja, maadhimisho ya kumbukumbu ya kuzaliwa Imam Mahdi (AS) aliyeahidiwa na Bwana Mtume Muhammad (SAW) kudhihiri katika zama za mwisho za dunia na kuujaza ulimwengu haki na uadilifu, yamefanyika kupitia matembezi ya amani.

Aidha Waislamu wamekusanyika tokea jana usiku kwenye kumbi, Misikiti na Husseiniya tofauti katika maeneo tofauti ya mji mkuu huo wa Nigeria, kuadhimisha siku hii tukufu, kwa kusikiliza mawaidha na nasaha za wanazuoni wa Kiislamu.

Katika jimbo la Yobe, Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, Waislamu hususan vijana wameadhimisha kumbukizi hii adhimu katika Kituo cha Kiislamu cha Markaz mjini Potiskum. Vijana wa Kiislamu waliokuwa wamevalia sare kama za maskauti wameghani mashairi na kusoma kasida za kumsifu Imam Mahdi AS.

Aidha maeneo tofauti ya Iran ya Kiislamu hususan katika miji mitakatifu ya Mash'had na Qum tangu jioni ya jana ilighariki katika sherehe za maadhimisho ya siku ya kuzaliwa mwokozi wa ulimwengu, Imam Zama, Mahdi (as).

Wapenzi wa Bwana Mtume Muhammad (SAW), Ahlul Bayt AS na Imam Mahdi AS wanaadhimisha siku ya kuzaliwa mtukufu huyo huku msikiti wa Jamkaran katika mjini Qum, (kusini mwa Tehran) ukiwa umefurika mamilioni ya Waislamu kutoka kona mbalimbali za dunia wakiwa na shauku kubwa ya kuona mwokozi huyo wa dunia akidhihiri haraka. 

Kwa mujibu wa wanahistoria, Imam Mahdi (AS), mwana wa Imam Hasan al Askari (AS) alizaliwa mjini Samarrah Iraq mwezi 15 Shaaban mwaka 255 Hijria. Baba wa mtukufu huyo yaani Imam Hasan al Askari (AS), ni Imam wa 11 wa Waislamu wa madhehebu ya Shia.