Jeshi la Kongo DR lashambuliana na waasi, mkoa wa Kivu Kusini
Duru za jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimeripoti kujiri mapigano baina ya jeshi la serikali na waasi katika mkoa wa Kivu Kusini, mashariki mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mapigano hayo yaliibuka baada ya askari wawili wa serikali waliokuwa wakipiga doria kwenye miinuko ya eneo la Kalehe, mkoani hapo kushambuliwa na waasi saba wa kundi linalofahamika kwa jina la Nyatura. Katika shambulizi hilo, askari hao walipoteza maisha. Waasi wa Nyatura walifanya shambulio hilo kama ulipizaji kisasi kufuatia muungano wa makundi ya waasi unaoyajumuisha makundi ya Mai-Mai, Kirikicho, Nyatura na Kifuafua kushindwa hivi karibuni katika operesheni za jeshi la serikali. Hadi sasa hakuna taarifa kamili iliyotolewa kufuatia mapigano hayo ya pande mbili. Maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yalitumbukia katika machafuko tangu miaka 20 iliyopita, machafuko ambayo yanasababishwa na uepo wa makundi ya waasi eneo hilo.