Wafuasi 5 wa Sheikh Zakzaky wauawa katika hujuma ya polisi, Kaduna, Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i95200-wafuasi_5_wa_sheikh_zakzaky_wauawa_katika_hujuma_ya_polisi_kaduna_nigeria
Askari usalama wa jimbo la Kaduna wamewaua watu wasiopungua 5 katika shambulizi dhidi ya wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN).
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 17, 2023 06:57 UTC
  • Wafuasi 5 wa Sheikh Zakzaky wauawa katika hujuma ya polisi, Kaduna, Nigeria

Askari usalama wa jimbo la Kaduna wamewaua watu wasiopungua 5 katika shambulizi dhidi ya wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN).

Muhammad Rabil, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo katika jimbo la Kaduna lililopo katikati mwa Nigeria amesema: Alhamisi ya jana karibu saa 4:00 jioni, wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria walifanya maandamano ya amani wakiitaka serikali ya Nigeria imrejeshee Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe pasi zao za kusafiria, ili waweze kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

Sheikh Ibrahim Zakzaky alijeruhiwa vibaya wakati wanajeshi wa Nigeria walipovamia Hussainia ya Baqiyatullah na nyumba ya mwanachuoni huyo katika mji wa Zaria mnamo Disemba 2015.

Katika shambulio hilo inakadiriwa wanachama zaidi ya 1,000 wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, aghalabu wakiwa Waislamu wa madhehebu ya Shia waliuawa kwa kufyatuliwa risasi na jeshi la Nigeria. Miongoni mwa waliouawa walikuwemo watoto watatu wa kiume wa Sheikh Ibrahim Zakzaky.

Ripoti zinasema, Gavana wa Jimbo la Kaduna, Nasiru El-Rufai akiwa pamoja na askari usalama wamewapiga risasi za moto waandamanaji hao katikka mji wa Kaduna na kuua watu wasiopungua 5 miongoni mwao. Waandamanaji wengine wengi wamejeruhiwa.

Gavana huyo wa jimbo la Kaduna alikuwa ameahidi kwamba iwapo atakubaliwa kugombea tena katika uchaguzi wa ugavana, atamaliza kazi ambayo haijakamilika ya kuwaangamiza Waislamu wa madhehebu ya Shia na Harakati ya Kiislamu katika jimbo la Kaduna.

Siku chache zilizopita pia wananchi wa Nigeria walifanya maandamano katika mji mkuu wa nchi hiyo, Abuja, kuishinikiza serikali impe Sheikh Ibrahim Zakzaky, pasipoti yake ya kusafiria.

Waandamanaji hao walikusanyika nje ya ofisi za Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Nigeria, ambapo walisikika wakipiga nara za kulaani hatua ya serikali ya kuendelea kuzuia pasi ya kusafiri ya Sheikh Zakzaky na mkewe Malama Zenat.

Kiongozi huyo wa kidini aliwekwa kizuizini katika mazingira magumu kwa zaidi ya miaka mitano licha ya hali yake mbaya ya kiafya, lakini hatimaye serikali ya Abuja ililazimika kumuachia huru kutokana na mashinikizo wananchi na jumuiya za kutetea haki za binadamu.