Ethiopia yaunda serikali ya mpito katika eneo la Tigray
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed ametangaza habari ya kuundwa serikali ya mpito katika eneo la Tigray la kaskazini mwa nchi, kama sehemu ya utekelezaji wa makubakubaliano ya amani.
Taarifa iliyotumwa jana Alkhamisi katika ukurasa wa Facebook wa Abiy Ahmed inasema, utawala huo wa kieneo wa mpito utaongozwa na mjumbe wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray TPLF, Getachew Reda.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa: Kulikuwa na haja ya kuundwa utawala jumuishi wa mpito ili kudhamini amani endelevu na kutamatisha mgogoro katika eneo hilo la kaskazini mwa nchi.
Serikali hiyo ya muda ya eneo la Tigray imeundwa siku moja baada ya Bunge la Ethiopia kuiondoa katika orodha ya makundi ya kigaidi Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray TPLF ya kaskazini mwa nchi hiyo.
Bunge hilo limesema lilichukua hatua hiyo ili kutoa fursa ya kutekelezwa makubaliano ya amani yaliyofikiwa mjini Pretoria Afrika Kusini kati ya serikali ya Addis Ababa na harakati ya TPLF.
Kwa mujibu wa makualiano hayo, mapigano yamesitishwa, huku huduma za msingi kama umeme, mawasiliano ya simu, benki,safari za ndege n.k zikianza tena huko Tigray kaskazini mwa Ethiopia.
Watu wasiopungua laki sita wameripotiwa kuuawa katika mapigano katika eneo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia, mbali na mamilioni ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi ndani ya nje ya nchi.