Uganda kutuma askari 1,000 nchini DRC mwezi huu
(last modified Fri, 24 Mar 2023 07:22:30 GMT )
Mar 24, 2023 07:22 UTC
  • Uganda kutuma askari 1,000 nchini DRC mwezi huu

Uganda imetangaza kuwa itapeleka wanajeshi elfu moja huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwezi huu, kama sehemu ya kikosi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Hayo yalitangazwa jana Alkhamisi na Kanali Mike Walaka Hyeroba, afisa wa Jeshi la Ulinzi la Uganda UPDF ambaye ameeleza kuwa, Uganda itatuma wanajeshi wake mashariki mwa DRC kufikia mwishoni mwa mwezi huu wa Machi, kwenda kupiga jeki mapambano dhidi ya waasi.

Kanali Hyeroba amesema wanajeshi hao wa Uganda watatumwa katika baadhi ya maeneo ambayo hivi sasa yanashikilia na kukaliwa na waasi wa M23 katika mkoa wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa Kongo DR.

Ikumbukwe kuwa, mwishoni mwa mwaka jana, Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC ilianza kupeleka wanajeshi wake huko mashariki mwa DRC, ili kuisaidia serikali ya Kinshasa kupambana na ongezeko la waasi wakiwemo wale wa M23.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa, tayari kuna vikosi vya Uganda vinavyoshirikiana na vya DR Congo katika operesheni ya pamoja dhidi ya waasi wa ADF mashariki mwa DRC tangu mwezi Desemba mwaka 2021. Hadi sasa wameshaua na kukamata mamia ya waasi hao, kwa mujibu wa taarifa ya kikosi hicho cha pamoja.

Wanajeshi wa Uganda UPDF

Waasi wa ADF walianzia uasi wao nchini Uganda katika miaka ya 1990 kwa shabaha ya kumpindua Rais Yoweri Museveni. Lakini walizidiwa nguvu na jeshi na kukimbilia kwenye misitu ya mashariki mwa Kongo ambako walishambulia vijiji, wakaua raia na kupora mali.

Mapigano katika jimbo la Kivu Kaskazini mbali na vifo, lakini pia yamesababisha idadi kubwa ya watu kuyakimbia makazi yao na kuzidisha mivutano ya kikanda, huku serikali ya DRC ikiishutumu Rwanda kwamba, inawaunga mkono waasi wa M23, madai ambayo yanakanushwa vikali na serikali ya Kigali ingawa yanaungwa mkono na madola ya Magharibi.

Tags