Oct 09, 2024 02:22 UTC
  • Jumatano, tarehe 9 Oktoba, 2024

Leo ni Jumatano tarehe 5 Rabiuthani 1446 Hijria inayosadifiana na Oktoba 9 mwaka 2024.

Katika siku kama ya leo miaka 179 iliyopita mwafaka na tarahe 5 Rabiuthani mwaka 1267 Hijiria, gazeti la kwanza la lugha ya Kifarsi lililoitwa 'Waqai'e Itifaqiyeh' lilianza kuchapishwa mjini Tehran.

Gazeti hilo lilianza kuchapishwa wakati wa kutimia mwaka wa tatu wa ufalme wa Nasiruddin Shah Kajjar, kwa amri ya Kansela Mirza Taqi Khan Amir Kabiri.

Gazeti hilo lilikuwa likiandika habari za utawala wa wakati huo wa Iran, dunia na makala za kisayansi zilizokuwa zikitafsiriwa kutoka kwenye magazeti ya Ulaya. Gazeti la 'Waqai'e Itifaqiyeh' lilichapisha hadi toleo nambari 472 na baada ya hapo liliendelea kuchapishwa kwa majina tofauti. *

Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, yaani tarehe 9 Oktoba 1962, nchi ya Uganda ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza.

Kuanzia mwaka 1890 Uganda ilikuwa chini ya makampuni ya Kiingereza yaliyokuwepo Afrika Mashariki, na baada ya kupita miaka kadhaa, ikatawaliwa rasmi na Uingereza. Baada ya kutawaliwa na mkoloni Muingereza, wananchi wa Uganda walipigania uhuru na hatimaye walifanikiwa kujipatia uhuru wao mwaka 1962 katika siku kama ya leo. 

Uganda yenye ukubwa wa kilomita mraba 235,880 kijiografia ipo mashariki mwa Afrika na inapakana nan chi za Sudan, Kenya, Tanzania, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Miaka 57 iliyopita katika siku kama ya leo, aliuawa Ernesto Che Guevara mwanamapinduzi mashuhuri wa Amerika ya Latini pamoja na wenzake kadhaa.

Che Guevara alizaliwa mwaka 1928 nchini Argentina. Fikra ya Ernesto Che Guevara ya kuendesha mapambano dhidi ya ubepari ilizidi kupanuka baada ya kushuhudiwa umaskini na ubaguzi uliotokana na siasa za kipebari za Marekani za kuyanyonya mataifa ya Amerika ya Latini. Ernesto che Guevara alifahamiana na Fidel Castro huko Mexico na viongozi hao wawili ndio walioongoza mapinduzi ya Cuba hadi kupatikana ushindi.

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Cuba mwaka 1959, Che Guevara alielekea Bolivia na kuasisi kundi la wapiganaji wa msituni. Alianza kupambana na serikali ya nchi hiyo iliyokuwa tegemezi kwa Marekani. Lakini katika siku kama ya leo mwaka 1967, wanajeshi wa Bolivia wakisaidiwa na shirika la ujasusi la CIA waligundua maficho ya Che Guevara na kumuuwa kwa kummiminia risasi.

Ernesto Che Guevara

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, Majid Abu Sharar, shakhsiya mwingine wa Palestina aliuawa na utawala haramu wa Israel huko nchini Italia. Abu Sharar ambaye alikuwa afisa wa kampeni wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO aliuawa na vibaraka wa shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel Mosad mjini Roma, Italia.

Israel imekuwa ikitumia njia ya kuwauwa kigaidi shakhsiya mbalimbali wa Palestina kama moja ya njia zake kuu za kusitisha mapambano ya ukombozi ya Wapalestina. 

Majid Abu Sharar

Na leo tarehe 9 Oktoba ni Siku ya Kimataifa ya Posta.

Posta ndio chombo cha kale zaidi na kikubwa cha mawasiliano baina ya wanadamu wa nchi na maeneo mbalimbali ya dunia. Taasisi hiyo ya posta ni miongoni mwa asasi za kijamii zilizobakia hai hadi leo.

Kutumiana ujumbe na barua ni miongoni mwa haja za kijamii za wanadamu tangu kiumbe huyu alipoanza maisha ya kijamii na posta ndiyo iliyokuwa chombo cha kukidhi mahitaji hayo kwa miaka mingi.   

 

Tags