Rais Kagame atangaza msamaha kwa shujaa wa "Hotel Rwanda"
Serikali ya Rwanda imemuachia huru Paul Rusesabagina, nyota wa filamu ya "Hotel Rwanda" aliyegeuka na kuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Rais Paul Kagame wa nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa jana Ijumaa na Wizara ya Sheria ya Rwanda imesema hukumu ya kifungo jela dhidi ya Rusesabagina imefutwa kwa amri ya rais, baada ya shujaa huyo wa 'Hotel Rwanda' kumuandikia barua Kagame akiomba msamaha.
Aidha Msemaji wa Serikali ya Rwanda, Yolande Makolo amethibitisha habari ya kupewa msahama Rusesabagina na kusisitiza kuwa, ameachiwa huru kutokana na ombi lake kwa Rais Paul Kagame wa nchi hiyo.
Ikumbukwe kuwa, Mahakama Kuu ya Rwanda mnamo Septemba mwaka 2021 ilimhukumiwa Rusesabagina kifungo cha miaka 25 jela baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya ugaidi kufuatia kesi ambayo waungaji mkono wake wanasema ilikuwa ya kimaonyesho na iliyochochewa kwa sababu za kisiasa.
Ilimhukumu kifungo hicho baada ya kumpata na hatia ya kujihusisha na kundi la waasi linalotuhumiwa kuhusika na mashambulio ya umwagaji damu ya utumiaji bunduki, maguruneti na uchomaji moto nchini humo katika miaka ya 2018 na 2019.
Jaji Beatrice Mukamurenzi wa mahaka hiyo alisema, Rusesabagina (68) aliunda shirika la kigaidi la National Liberation Front (FLN) lililoishambulia Rwanda, na akachangia kifedha pia kufadhili harakati za kigaidi.
Muda mfupi baada ya kutiwa mbaroni mnamo Agosti 2020, wanaharakati na watetezi wa kimataifa wa haki za binadamu walidai kuwa Rusesabagina ametekwa nyara na kwamba maisha yake yamo hatarini.
Mwishoni mwa mwaka jana, Rais Kagame aliikosoa vikali Marekani kwa kuishinikiza serikali ya Kigali imuachie huru nyota huyo wa filamu ya "Hotel Rwanda" aliyegeuka na kuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Kigali.