Miili 19 ya Waethiopia yapatikana kwenye lori DRC
Miili ya raia 19 wa Ethiopia waliofariki dunia kwa kukosa hewa ndani ya lori moja la mizigo la Zambia imepatikana kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ufwa Kasongo Kibali, Waziri wa Mambo ya Ndani wa mkoa wa Haut Katanga, kusini mashariki mwa Kongo DR amesema vyombo vya usalama viligundua miili hiyo baada ya kusimamisha lori hilo kwa ajili ya upekuzi katika mji wa Mwenda, karibu na mpaka na Zambia.
Amesema kuwa raia wengine 76 wa Ethiopia wamepatikana wakiwa hai ndani ya lori hilo la mizigo la Zambia. Idhaa ya Umoja wa Mataifa ya Radio Okapi imetangaza kuwa yumkini walioaga dunia walikuwa wahamiaji kutoka nchi kadhaa za Kiafrika wakilekea Afrika Kusini. Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imewakabidhi raia waliopatikana hai kwa ubalozi mdogo wa Zambia nchini humo.
Itakumbukwa kuwa, raia 45 wa Ethiopia walipatikana wameaga dunia ndani ya shehena iliyokuwa kwenye lori la mizigo kwa kukosa hewa katikati mwa Tanzania mnamo Juni mwaka 2012.