UN yaituhumu EU kuunga mkono jinai dhidi ya binadamu Libya
(last modified Tue, 28 Mar 2023 07:25:10 GMT )
Mar 28, 2023 07:25 UTC
  • UN yaituhumu EU kuunga mkono jinai dhidi ya binadamu Libya

Jopo la uchunguzi la Umoja wa Mataifa limesema kwamba, kuna ushahidi unaoonyesha kuwa jinai dhidi ya binadamu zimefanywa dhidi wa wananchi wa Libya na wahajiri waliokwama katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, wakiwemo wanawake wanaolazimishwa kuingia kwenye utumwa wa kingono.

Timu ya uchunguzi ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa imeubebesha dhima Umoja wa Ulaya na kuutaja kuwa sehemu ya jinai hizo dhidi ya Walibya na wahamiaji, kwa kutuma misaada na kuviunga mkono vikosi vya usalama vya Libya.

Wachunguzi wa UN wamesema wanatiwa wasiwasi mkubwa na hali mbaya ya kibinadamu na kudodora kwa haki za binadamu nchini Libya, wakisisitiza kuwa kuna msururu mkubwa wa jinai zinazofanywa na maafisa usalama na makundi ya mamluki yaliyojizatiti kwa silaha nchini humo.

Chaloka Beyani, mmoja wa wachunguzi hao wa UN ameiambia televisheni ya al-Jazeera kuwa, wamekusanya simulizi, ushahidi na taarifa 2,800 zinaoonesha ukubwa wa jinai zinazofanyika nchini Libya, kama vile mauaji, kamatakamata kinyume cha sheria, utesaji, ubakaji, utumwa, utumwa wa kingono na watu kupotezwa.

Mwaka 2021 wahajiri 32,425 walikamatwa na maafisa usalama kwa mashinikizo ya EU na kurejeshwa kwa nguvu Libya, ambapo 662 walifariki dunia na 891 walitoweka, wakati walipopanda boti dhaifu na kujaribu kuvuka Bahari ya Meditarrenean kuelekea barani Ulaya.

Wahajiri wanavyofia majini katika safari hatarishi za kwenda Ulaya

Libya yenye utajiri wa mafuta imesalia katika machafuko tangu 2011, wakati mtawala wa muda mrefu Muammar Gaddafi alipoondolewa madarakani na waasi walioungwa mkono na muungano wa kijeshi wa nchi za Magharibi, NATO.

Mwishoni mwa mwaka uliopita wa 2022, ripoti mpya iliyotolewa na shirika moja la kutetea haki za binadamu ilifichua kuwa, maelfu ya wahajiri walipewa kichapo cha mbwa, baadhi wakadhalilishwa na wengine wakazuiliwa kinyume cha sheria kabla ya kurejeshwa waliokotoka na askari wa mipaka ya nchi za Umoja wa Ulaya.

 

Tags