Kuongezeka idadi ya wahajiri wa Kiafrika wanaoelekea Ulaya
Taasisi ya kudhibiti na kusimamia mipaka ya nchi za Ulaya, imetabiri kuwa katika miezi ijayo karibu kila wiki jumla ya wahajiri elfu 10 kutoka nchi za Kiafrika wataingia barani humo kupitia bahari ya Mediterranean.
Kwa mujibu wa taarifa ya taasisi hiyo, karibu wahajiri laki tatu wataingia barani Ulaya kwa kutumia usafiri wa boti ndani ya mwaka huu pekee wa 2016. Gazeti la Kijerumani la Bild Zeitung limemnukuu katibu mtendaji wa taasisi hiyo ya kudhibiti na kusimamia mipaka ya nchi za barani Ulaya akisema kuwa, inatarajiwa kuwa karibu kila wiki jumla ya wahajiri elfu 10 wataingia Ulaya kupitia nchi ya Libya ya kaskazini mwa Afrika. Kufuatia hali hiyo, Shirika la Kimataifa la Wakimbizi, limeunga mkono taarifa ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani kuhusiana na suala hilo. Hivi karibuni Thomas de Maizière, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani alinukuliwa akisema kuwa, karibu watu milioni moja kutoka nchi inayokumbwa na vita ya Libya, wamejiandaa kufanya safari kuelekea barani Ulaya. De Maizière ameashiria pia magenge yanayojishughulisha na magendo ya binaadamu ambayo yamebobea katika shughuli hizo za kuwasafirisha wahajiri kuelekea Ulaya. Magenge hayo hutumia boti ndogo na hatari, kuvusha idadi kubwa ya wahajiri kwenda barani Ulaya. Viongozi wa magenge hayo huchukua hatua hiyo kwa kuamini kuwa, endapo zitazama ndani ya bahari ya Mediterranea na pwani ya Italia na Ugiriki, basi abiria wataokolewa na meli za doria za nchi wanachama wa EU. Pamoja na kwamba baadhi hufanikiwa kufika salama huko waendako, lakini hadi sasa idadi kubwa ya wahamiaji hao haramu wamepoteza maisha katika safari hizo za kuelekea barani Ulaya. Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, hadi kufikia katikati ya mwezi Juni mwaka huu, karibu wahamiaji haramu elfu 50 kutoka nchi za Kiafrika waliwasili na boti hizo katika pwani ya Italia. Takwimu rasmi zinaonyesha kwamba kwa akali nusu nzima ya wahajiri hao waliowasili barani Ulaya mwaka jana, wanatoka nchi za Kiafrika. Kwa mujibu wa ripoti hiyo idadi ya wahajiri haramu wa Kiafrika waliowasili barani Ulaya kati ya kipindi cha kati ya mwezi Januari na Novemba mwaka 2015, kimeongezeka mara sita zaidi ikilinganishwa na idadi ya mwaka 2014. Wahajiri hao haramu ambao kutokana na sababu za kiuchumi huamua kuziacha nchi zao kwa tamaa ya kwenda kutafuta kazi na maisha mazuri barani Ulaya, hutokea nchi za Nigeria, Eritrea, Somalia, Sudan, Gambia, Senegal, Mali, Morocco na Tunisia. Kuongezeka wahajiri hao kutoka Nigeria na Somalia, kunatokana na khofu ya mashambulizi ya wanachama wa makundi ya kigaidi na kitakfiri ya Boko Haram na ash-Shabab, makundi ambayo ni maarufu kwa kufanya jinai dhidi ya binaadamu. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana idadi ya wahajiri wa Nigeria nchini Italia ndani ya kipindi cha mwaka mmoja pekee, ikaongezeka mara tatu zaidi. Hivi sasa kuna wasi wasi kwamba makundi ya kigaidi kama vile Boko Haram ambalo lilitangaza utiifu wake kwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh, huenda yakatumia mwanya wa wahajiri wanaoenda Ulaya kuchanganyika nao na kuweza kuingia barani humo. Kwa mtazamo wa weledi wa mambo, mgogoro wa wakimbizi haramu ambao ulishadidi mwaka mmoja uliopita, umeandaa mazingira mazuri kwa wanachama wa makundi ya kigaidi ya ash-Babab na Boko Haram kuingia Ulaya. Ni kufuatia hali hiyo ndio maana katika kikao cha pamoja cha bara la Afrika na Ulaya kilichofanyika mwezi Novemba mwaka jana huko mjini Malta, Rais Macky Sall wa Senegal akasema bayana kwamba kiwango cha Euro bilioni moja na milioni 300 ambazo zimetengwa na nchi za Ulaya kwa ajili ya nchi za Kiafrika, ni kidogo sana na kisichotosha. Viongozi wa nchi za Ulaya walitenga kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya viongozi wa Kiafrika ili waweze kuwazuia wahajiri haramu wa nchi zao kwenda Ulaya.