Wakimbizi wa Eritrea wapokea msaada wa kimatibabu Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i9595-wakimbizi_wa_eritrea_wapokea_msaada_wa_kimatibabu_ethiopia
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka limeanza kuwapa msaada wa kimatibabu wakimbizi wa Eritrea ambao wamekimbilia Ethiopia kutokana na kushtadi mapigano mpakani mwa nchi mbili hizo jirani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 20, 2016 02:41 UTC
  • Wakimbizi wa Eritrea wapokea msaada wa kimatibabu Ethiopia

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka limeanza kuwapa msaada wa kimatibabu wakimbizi wa Eritrea ambao wamekimbilia Ethiopia kutokana na kushtadi mapigano mpakani mwa nchi mbili hizo jirani.

Oliver Schultz, Mkuu wa shirika hilo nchini Ethiopia amesema kuna maelfu ya wakimbizi wa Eritrea wanaohitaji misaada ya dharura katika kambi za wakimbizi kaskazini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika na kwamba kwa sasa madaktari wa shirika hilo la kimataifa wanaendelea kuwapa matibabu ya kimwili na kisaikolojia wakimbizi hao.

Wizara ya Habari ya Eritrea hivi karibuni ilitangaza kwamba askari jeshi wa nchi hiyo wameua zaidi ya askari 200 wa Ethiopia na kuwajeruhi wengine zaidi ya 300 katika makabiliano makali zaidi kuwahi kuripotiwa kati ya nchi hizo tokea kumalizika kwa mapigano ya mwaka 1998 hadi 2000.

Hii ni katika hali ambayo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameelezea wasiwasi wake kutokana na mapigano ya mpakani kati ya Ethiopia na Eritrea. Ban Ki-moon amezitaka Addis Ababa na Asmara kujiepusha na hatua zozote zinazoshadidisha hali ya mivutano kati ya nchi mbili hizo na kusisitiza kuwa, nchi hizo jirani zinapasa kutatua hitilafu zao kwa njia ya amani na kutekeleza makuballiano ya amani yaliyosainiwa na nchi mbili hizo mwaka 2000. Ethiopia na Eritrea zimewahi kuingia vitani tena kutokana na mzozo wa mpaka kuanzia mwaka 1998 hadi 2000, ambapo watu zaidi ya 80,000 waliuawa.