IMN yazienzi familia za Mashahidi wa njia ya Muqawama wa nchini Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i96434-imn_yazienzi_familia_za_mashahidi_wa_njia_ya_muqawama_wa_nchini_nigeria
Harakati ya Kiislamu ya Nigeria IMN inayoongozwa na Sheikh Ibrahim Zakzaky siku ya tarehe 27 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ilifanya hafla ya kuzienzi na kuzipongeza familia za mashahidi wa Siku ya Quds Duniani na wa maandamano ya Ashura nchini humo.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Apr 19, 2023 03:02 UTC

Harakati ya Kiislamu ya Nigeria IMN inayoongozwa na Sheikh Ibrahim Zakzaky siku ya tarehe 27 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ilifanya hafla ya kuzienzi na kuzipongeza familia za mashahidi wa Siku ya Quds Duniani na wa maandamano ya Ashura nchini humo.

Katika miaka ya hivi karibuni, jeshi la Nigeria limeshambulia maandamano ya amani ya Siku ya Quds Duniani na Siku ya Ashura (Mauaji ya Zaria), na kuwaua shahidi na kuwajeruhi mamia ya wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria na waungaji mkono wa harakati hiyo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, Harakati ya Kiislamu ya Nigeria jana ilizialika familia za Mashahidi wa njia ya Muqawama kwenye futari maalumu katika baadhi ya miji ya nchi hiyo ukiwemo wa Bauchi, na kuzienzi na kuzipongeza familia hizo za Mashahidi.
Sheikh Yusuf Ahmad Yashi, mwakilishi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky katika jimbo la Bauchi amehutubia dhifa hiyo ya futari kwa ajili ya familia za Mashahidi wa njia ya Muqawama na kueleza kwamba: "Muqawama ni jambo la lazima katika kukabiliana na watumiaji mabavu na nchi za Kibeberu".
Sheikh Ibrahim Zakzaky

Abdul Qadir Giladi, mmoja wa wazazi wa Mashahidi wa muqawama, amemueleza ripota wa Iran Press: Hatua ya Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ya kuzienzi familia za Mashahidi inaonyesha mshikamano wao na Mashahidi na inapasa kuheshimiwa.

Kitambo nyuma, katika muendelezo wa ukandamizaji na mauaji ya Waislamu wa madhehebu ya Shia, vikosi vya usalama vya Jimbo la Kaduna viliua watu wasiopungua sita katika shambulio dhidi ya wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.
Mauaji hayo yalitokea baada ya wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria kufanya maandamano ya amani na kuitaka serikali ya Nigeria iachie hati ya kusafiria ya kimataifa ya Sheikh Zakzaky na mkewe ili waweze kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kupatiwa huduma za matibabu.../