Makumi ya wanajeshi wa Burkina Faso wauawa katika shambulizi mashariki mwa nchi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i96756-makumi_ya_wanajeshi_wa_burkina_faso_wauawa_katika_shambulizi_mashariki_mwa_nchi
Wanajeshi 33 wa jeshi la Burkina Faso waliuawa jana baada ya wanamgambo wenye silaha kuvamia kituo cha jeshi mashariki mwa nchi hiyo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Apr 28, 2023 03:41 UTC
  • Makumi ya wanajeshi wa Burkina Faso wauawa katika shambulizi mashariki mwa nchi

Wanajeshi 33 wa jeshi la Burkina Faso waliuawa jana baada ya wanamgambo wenye silaha kuvamia kituo cha jeshi mashariki mwa nchi hiyo.

Jeshi la Burkina Faso limesema kuwa shambulizi hilo lilitekelezwa na magaidi katika kituo cha kijeshi huko Ougarou  mashariki mwa nchi hiyo. Taarifa ya jeshi la Burkina Faso imeeleza kuwa wanajeshi waliokuwa wamezingirwa katika kituo hicho walifanikiwa kuwauwa magaidi 40 kabla ya askari wa usaidizi kuwasili.

Burkina Faso ni moja ya nchi kadhaa za Magharibi mwa Afrika zinaoendesha mapambano dhidi ya makundi ya wanamgambo wenye silaha wanaoendesha hujuma na mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya raia na vikosi vya jeshi.

Burkina Faso na hujuma za makundi yenye silaha 

Hujuma hizo za wanamgambo wenye silaha zimeenea hadi katika nchi jirani ya Mali kwa muongo mmoja sasa; ambapo maelfu ya watu wameuawa na wengine zaidi ya milioni mbili wamekuwa wakimbizi. Mashambulizi  ya magaidi wenye silaha dhidi ya jeshi la Burkina Faso yameongezeka katika miezi ya karibuni huku serikali ikifanya juhudi za kuyaangamiza makundi hayo ya waasi.