Mahakama Misri yabatilisha kukabidhiwa Saudia visiwa viwili muhimu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i9676-mahakama_misri_yabatilisha_kukabidhiwa_saudia_visiwa_viwili_muhimu
Mahakama moja nchini Misri imetengua hatua ya serikali ya Rais Abdulfattah al-Sisi wa nchi hiyo ya kuipatia Saudi Arabia visiwa viwili vya kistratejia vya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 21, 2016 10:25 UTC
  • Mahakama Misri yabatilisha kukabidhiwa Saudia visiwa viwili muhimu

Mahakama moja nchini Misri imetengua hatua ya serikali ya Rais Abdulfattah al-Sisi wa nchi hiyo ya kuipatia Saudi Arabia visiwa viwili vya kistratejia vya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Hukumu hiyo ya muda imetolewa kufuatia hatua ya wananchi na wanaharakati kuwasilisha kesi mahakamani hapo kupinga uamuzi wa serikali wa kuipatia serikali ya Riyadh visiwa vyake viwili vya Sanafir na Tiran vilivyoko kwenye Ghuba ya Aqabah katika Bahari Nyekundu.

Uamuzi huo ni pigo kwa Rais Abdulfattah al-Sisi, ambaye hivi karibuni alilihutubia taifa akiwataka wananchi kusitisha maandamano na lalama zao juu ya suala la visiwa hivyo. Hata hivyo serikali ya Cairo iko huru kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa, hatua ya al-Sisi kuipatia Saudia visiwa hivyo ilikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wananchi. Kisiwa cha Tiran kina upana wa kilomita mraba 80 katika lango la Tiran na Ghuba ya Aqabah, huku kile cha Sanafir kikiwa na ukubwa wa karibu kilomita mraba 33.

Rais Rais Abdulfattah al-Sisi wa Misri alimpatia Mfalme Salman bin Abdulaziz wa Saudia visiwa vya Sanafir na Tiran na kudai kuwa, michoro ya kimipaka baharini inaonyesha kwamba, visiwa hivyo vilivyoko Bahari Nyekundu viko katika maji ya Saudia. Iliarifiwa kuwa, serikali ya Misri ilipokea dola bilioni 20 za Marekani kutoka utawala wa Aal-Saud ili kuuuzia visiwa hivyo, ambavyo ni milki ya nchi hiyo ya Kiafrika.