Serikali ya Uingereza yazidi kukosolewa kwa kuiuzia Saudia silaha
Matokeo ya utafiti uliofanywa na Umoja wa Mataifa kuhusiana na mashambulizi makubwa yanayofanywa na Saudi Arabia dhidi ya raia huko Yemen yamezidisha mashinikizo kwa serikali ya Uingereza kutokana na hatua yake ya kuiuzia silaha Riyadh.
Gazeti la The Guardian la nchini Uingereza limeandika kuwa, ripoti hiyo yenye kurasa 51 ambayo wiki iliyopita iliwasilishwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lakini bado haijasambazwa, inaashiria mashambulizi ya Saudi Arabia na waitifaki wake dhidi ya raia wasio na hatia wa Yemen.
Saudi Arabia ambayo ni moja ya nchi wanunuzi wakubwa wa silaha kutoka Uingereza, ilianzisha mashambulizi ya kijeshi huko Yemen tangu mwezi Machi mwaka jana huku ikiungwa mkono na nchi kadhaa waitifaki wake.
Makundi ya kutetea haki za binadamu yameripoti kuhusu Uingereza kuiuzia Saudia kwa wingi silaha na zana za kijeshi, sambamba na kuongezeka mashambulizi ya muungano vamizi unaoongozwa na nchi hiyo huko Yemen. Ripoti ya Amnesty International imefichua kuwa kuanzia mwezi Julai hadi Septemba mwaka jana, Uingereza iliiuzia Saudia silaha za thamani ya pauni bilioni moja na milioni 66.