May 08, 2023 06:25 UTC
  • Mwanasiasa wa Morocco:  Kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel ni usaliti

Mmoja wa viongozi wa kisiasa wa harakati za mrengo wa kushoto nchini Morocco ametangaza kuwa, kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel ni khiyana na usalitii mkubwa kwa sasa na kwa baadaye kwa Morocco na taifa lolote lile la Kiarabu.

Nabil Manib, Katibu Mkuu wa chama cha kisoshalisti cha muungano wa Morocco amesema hayo katika mkutano wa tatu Baraza la Kambi ya Morocco Kwa Ajili ya Kuunga Mkono Palestina na kupinga kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel na kueleza kwamba, mchakato wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel ulianza miongo kadhaa iliyopita kupitia Shirika la Ujasusi la Israel Mossad.

Mwanasiasa huyo wa Morocco amewataka Wabunge wa nchi hiyo wajadidishe upinzani wao dhidi ya hatua ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel.

Desemba 2020, Morocco na utawala haramu wa Israel zilifikia mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida kwa ushawishi wa Marekani. Na kama sehemu ya makubaliano hayo, Rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump alikubali kutambua mamlaka ya Morocco juu ya Sahara Magharibi. Hata hivyo serikali ya rais wa sasa wa nchi hiyo Joe Biden imesema itauangalia upya uamuzi huo.

Mara kwa mara, wananchi wa Morocco wamekuwa wakifanya maandamano ya kupinga na kulaani hatua ya utawala wa kifalme wa nchi hiyo ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Maandamano hayo yanafanyika huku Morocco na Israel zikiendelea kufikia mapatano ya pande mbili katika nyanja za kijeshi, kiuchumi na kielimu na wakati huo huo Israel ikishadidisha mashambulizi na ukandamizaji dhidi ya raia wa Palestina.

Tags