Watu 15 waaga dunia baada ya boti kuzama Nigeria; 25 hawajulikani walipo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i97238-watu_15_waaga_dunia_baada_ya_boti_kuzama_nigeria_25_hawajulikani_walipo
Sanusi Abubakar msemaji wa polisi katika jimbo la Sokoto nchini Nigeria ameripoti kuwa watu 15 wamepoteza maisha baada ya boti kuzama Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 11, 2023 11:23 UTC
  • Watu 15 waaga dunia baada ya boti kuzama Nigeria; 25 hawajulikani walipo

Sanusi Abubakar msemaji wa polisi katika jimbo la Sokoto nchini Nigeria ameripoti kuwa watu 15 wamepoteza maisha baada ya boti kuzama Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo.

Boti hiyo ilikuwa ikielekea katika kijiji cha Dundeji katika jimbo la Sokoto wakati ilipozama katikati ya mto. Jumla ya watu 36 walikuwa wamepanda boti hiyo; ambapo 21 kati yao wameokolewa. Wanawake 13 na wanaume wawili ndio walioaga dunia. 

Wanakijiji cha Dunjeji jimboni Sokoto wamekusanyika kuwaomboleza wapendwa wao waliopoteza maisha katika ajali hiyo ya boti ambao walikuwa katika safari ya kutafuta kuni. Umar Yobo mwakilishi wa serikali za mitaa amevitaja vifo hivyo kuwa pigo kubwa kwa jamii ya Dunjeji, yapata umbali wa kilomita 55 kutoka makao makuu ya jimbo la Sokoto. 

Mamlaka husika katika jimbo la Sokoto tayari zimeanzisha uchunguzi kuhusu ajali hiyo ya boti.

Ikumbukwe kuwa ajali za kuzama boti zimekuwa zikitokea mara kwa mara katika maeneo mengi yanayozungukwa na mito huko Nigeria; ambako boti za kienyeji hutumika pakubwa kama njia kuu za usafiri. Ajali hizo aidha zinatajwa kusababishwa na idadi kubwa ya watu wanopanda na utumiaji wa boti pasina kuzitunza vizuri.