Kwa akali watu 30 wameuawa katika mashambulizi kaskazini mwa Nigeria
Watu waliokuwa na silaha wameshambulia vijiji kadhaa katika jimbo la Plateau hujko nchini Nigeria na kupelekea mauaji ya watu wasiopungua 30.
Hiyo ni kwa mujibu wa mamlaka husika nchini Nigeria ambazo zimeeleza kuwa, makkumi ya watu wamejeruhiwa pia katika mashambulio hayo.
Maeneo ya kaskazini magharibi na katikati mwa Nigeria kwa muda mrefu yamekuwa yakishuhudia mapigano kati ya wakulima na wafugaji wakigombea maji, ardhi pamoja na malisho ya mifugo. Mgogoro wa usalama katika maeneo hayo umesababisha maelfu ya vifo.
Washambuliaji hao walilenga vijiji vitatu katika eneo la Mangu katika jimbo la Plateau.
Gavana wa Plateau Simon Lalong amesema amesikitishwa na shambulio hilo na kuviagiza vikosi vya usalama kuwasaka washukiwa wa shambulio hilo.
Mgogoro wa usalama wa Nigeria unatarajiwa kuwa changamoto kubwa kwa rais mteule Bola Tinubu, ambaye anatarajiwa kuchukua madaraka baadaye mwezi huu.
Mbali na mauaji yanayosababishwa na ugomvi wa maji na ardhi, Nigeria inakabiliwa pia na hujuma ya kundi la kigaidi la Boko Haram ambalo limehatarisha usalama katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Kundi la kigaidi la Boko Haram lilishika silaha mwaka 2009 kwa lengo la kile lilichotaja kuwa, kuwa huru eneo la kaskazini mwa Nigeria; na kuanzia hapo likaanza kueneza jinai na mashambulizi yake huko Niger, Chad na kaskazini mwa Cameroon.
Tangu wakati huo hadi sasa kundi hilo limeua watu wapatao 36 elfu na kusababisha raia wengine zaidi ya milioni mbili pia kuwa wakimbizi katika nchi hizo za magharibi mwa Afrika.