May 26, 2023 09:54 UTC
  • AU yaonya: Afrika isigeuzwa uwanja wa kutunishiana misuli madola makubwa

Viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) wameyaonya madola makubwa duniani hasa ya Magharibi dhidi ya kuligeuza bara la Afrika kuwa medani ya malumbano na kutununishiana misuli, wakati huu ambapo baadhi ya nchi za bara hilo zinakabiliwa na changamoto za kiusalama.

Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU alisema hayo jana Alkhamisi mjini Addis Ababa, Ethiopia katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Afrika na kusisitiza kuwa, Afrika haitashurutishwa kuegemea upande wowote katika vita na mapigano yanayoendelea nchini Ukraine.

Mahamat amesema, "Katika muktadha huu wa kimataifa wa kulumbana pande zenye maslahi na misimamo kinzani ya kisiasa, azma ya kila upande inatishia kuligeuza bara Afrika kuwa medani ya jiostratejia, na hivyo kuibua Vita Baridi vipya."

Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU ameeleza bayana kuwa, nchi wanachama wa Umoja wa Afrika zinapasa kuwa macho ili zisijikute zimelazimishwa kujiunga na upande fulani kwenye mgogoro wa Ukraine, ambapo bara hilo halitaambulia chochote. 

Hapo jana bara la Afrika liliadhimisha miaka 60 ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) na taasisi iliyoundwa baada yake, yaani Umoja wa Afrika (AU). Viongozi wa Afrika wamekuwa wakikosoa siasa za kikoloni za nchi za Magharibi katika nchi za Afrika wakisisitiza kuwa Wamagharibi hawataki kuwapo utulivu wa kisiasa katika nchi hizo ili kupora rasilimali na utajiri wake na kuzuia ustawi na maendeleo.

Mwenyekiti wa sasa wa AU, ambaye pia ni Rais wa Comoro, Azali Assoumani

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa sasa wa AU, ambaye pia ni Rais wa Comoro, Azali Assoumani amekosoa mapinduzi haramu na yanayokanyaga katiba yaliyoshuhidiwa karibuni katika nchi kadhaa za Afrika.

Ameashiria mapigano yanayoendelea nchini Sudan na kusisitiza kuwa, "Tunapasa kuwashawishi ndugu zetu wa Sudan kukumbatia mazungumzo ili vita haribifu vinavyoshuhudiwa nchini humo vimalizike."

Tags