Jun 02, 2023 02:12 UTC
  • Human Rights Watch: Dhulma zaendelea kushuhudiwa katika jimbo la Tigray Ethiopia

Shirika la Haki za Binadamu ya Huma Rights Watch limezishutumu mamlaka za ndani na vikosi vya jimbo la Amhara kuendelea kuwafukuza kwa lazima Watigray, kama sehemu ya kampeni ya safishasafisha ya kikabila magharibi mwa Tigray licha ya mapatano.

Human Rights Watch imesema katika ripoti yake iliyochapishwa jana kwamba tangu kuzuka mzozo na mapigano katika jimbo la Tigray Novemba 2020, vikosi vya usalama vya Amhara pamoja na uongozi wa muda wameendesha kampeni ya takasatakasa ya kikabila dhidi ya jamii ya wa Tigray magharibi mwa jimbo la Tigray, wakitenda uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.

Utafiti wa karibuni wa shirika hilo umegundua kuwa, maafisa wawili, Kanali Demeke Zewdu na Belay Ayalew, waliolaumiwa huko nyuma kwa kutenda dhulma, wanaendelea kuhusika katika ukamataji wa holela, mateso, na uhamishaji wa lazima wa Watigray.

Naibu mkurugenzi wa Afrika wa Human Rights Watch Laetitia Bader, amesema, mapatano ya Novemba ya Ethiopia Kaskazini hayajahitimisha madhila kwa jamii ya Watigranya katika zoni ya magharibi ya Tigray, na kuitaka serikali ya Ethiopia kuacha kuzuia uchunguzi huru kuhusu ukatili uliofanywa huko, kuwawajibisha makamanda na maafisa waiohusika, ikiwa kweli inataka kuhakikisha haki inatendeka. 

Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) ilipigana na vikosi vya serikali ya Ethiopia na waitifaki wao katika vita vilivyouwa makumi ya maelfu ya watu katika eneo la Tigray. Makubaliano ya amani kati ya pande mbili yalifikiwa mwezi Novemba mwaka jana baada ya jeshi la Ethiopia kupata ushindi mara kadhaa dhidi ya TPLF.