Kikosi cha kikanda chaongezewa muda wa kubakia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Kikosi cha kikanda kilichoundwa ili kukabiliana na ghasia za wanamgambo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kimeongezewa muda wa kubakia katika nchi hiyo.
Duru kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zinasema kuwa, sasa kikosi hicho kitabakia nchini humo hadi Septemba mwaka huu baada ya kuongezewa muda.
Nchi saba za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zilianzisha kikosi cha kijeshi cha EACRF mwezi Aprili mwaka jana ili kujaribu kumaliza umwagikaji wa damu unaohusishwa na miongo kadhaa ya shughuli za wanamgambo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mustakabali wa kikosi hicho ulikuwa haujulikani tangu muda wake ulipomalizika mwezi Machi, na viongozi wa EAC walikuwa wametoa maoni tofauti kuhusu jinsi kinavyopaswa kufanya kazi.
Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amekuwa akikosoa utendaji wa kikosi hicho.
Akizungumza wakati wa ziara yake nchini Botswana, Tshisekedi aliesema ana wasiwasi na alichokiita “kuishi pamoja” waasi na kikosi hicho cha Afrika Mashariki ambacho kilianza kupelekwa DRC mwishoni mwa mwaka jana. Makundi mengi yenye silaha yanavuruga usalama Mashariki mwa DRC ambako Kundi la M23, lilianzisha mashambulizi tangu lilipoibuka tena baada ya kusambaratika mwishoni mwa mwaka 2021.
Kufuatia matamshi hayo, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ilimtaka Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuheshimu hatua ya mataifa ya kikanda ya kupeleka vikosi katika jaribio la kuleta utulivu katika maeneo ya mashariki mwa nchi yake.