UN yataka uchaguzi mkuu DRC ufanyike mwishoni mwa mwaka huu
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limebainisha wasiwasi wake kuhusu kukamatwa kiongozi wa upinzani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, na limetaka uchaguzi wa rais nchini humo ufanyika mwishoni mwa mwaka huu kama inavyotakiwa na katiba ya nchi hiyo.
Serikali ya DRC imesema haitaweza kuandaa uchaguzi katika muda uliopangwa kutokana na matatizo ya usimamizi huku wapinzani wa Rais Joseph Kabila wakimtuhumu kuwa anapanga njama ya kuendelea kubakia madarakani.
Kabila, ambaye aliingia madarakani mwaka 2001, anazuiwa na katiba kuwania urais kwa muhula wa tatu katika uchaguzi ulipangwa kufanyika Novemba. Imedokezwa kuwa Kabila anapanga kuitisha kura ya maoni ili awaulize wananchi waamue iwapo agombee urais au la.
Katika azimio la Alkhamisi, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesisitiza kuhusu kulindwa haki za kimsingi ili kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi huru, wenye itibari, wa wazi, unaojumuisha wote na kwa wakati ulioainishwa na katiba, yaani Novemba 2016, hasa chaguzi za bunge na rais.
Hayo yanajiri wakati ambao wiki hii mahakama moja katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilimhukumu miaka mitatu jela, kinara wa upinzani nchini humo ambaye pia ni mgombea wa urais katika uchaguzi mkuu ujao, Moise Katumbi, aliyekuwa anakabiliwa na tuhuma za mauzo ya nyumba kinyume cha sheria.