Rais wa Nigeria awataka wananchi kuwa watulivu kufuatia kuondolewa ruzuku ya mafuta
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i98714-rais_wa_nigeria_awataka_wananchi_kuwa_watulivu_kufuatia_kuondolewa_ruzuku_ya_mafuta
Rais Bola Tinubu wa Nigeria jana aliwatolea wito wananchi kukubali kujitolea zaidi kwa ajili ya uwekezaji wa baadaye baada ya serikali yake kuhitimisha ruzuku ya muda mrefu ya mafuta katika hatua ambayo imesababisha kupanda kwa bei ya petroli, usafiri na vyakula nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 13, 2023 04:39 UTC
  • Rais wa Nigeria awataka wananchi kuwa watulivu kufuatia kuondolewa ruzuku ya mafuta

Rais Bola Tinubu wa Nigeria jana aliwatolea wito wananchi kukubali kujitolea zaidi kwa ajili ya uwekezaji wa baadaye baada ya serikali yake kuhitimisha ruzuku ya muda mrefu ya mafuta katika hatua ambayo imesababisha kupanda kwa bei ya petroli, usafiri na vyakula nchini humo.

Tinubu ambaye alichaguliwa kuwa Rais wa Nigeria mwezi Februari mwaka huu katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali alisema katika siku yake ya kwanza akiwa kazini mwezi uliopita kwamba anahitimisha ruzuku ya mafuta ambayo imeigharimu serikali mabilioni ya dola ili kujaribu kuteremsha bei ya mafuta nchini. Itakumbukwa kuwa Nigeria ni mojawapo ya wazalishaji wakubwa wa mafuta barani Afrika lakini ina uwezo mdogo wa kusafisha mafuta.

Rais wa Nigeria ahitimisha ruzuku ya mafuta 

Kwa miongo kadhaa sasa Nigeria imebadilisha mafuta ghafi kwa petroli na hivyo kusababisha upungufu mkubwa wa mapato, fedha za kigeni na kuongezeka deni la nchi hiyo. AKihutubia taifa kwa njia ya televisheni  katika maadhimisho ya Siku ya Demokrasia ya Nigeria, Rais Bola Tinubu ameeleza kuwa kuhitimisha utoaji wa ruzuku ni hitaji chungu kwa ustawi wa uchumi wa nchi hiyo." Kwa masikitiko, nawaomba wananchi mjitolee kwa ajili ya ustawi wa nchi; na kwa imani yenu nawahakikishia kwamba kujitoa kwenu huku hakutapotea bure, amesema Rais Bola Tinubu wa Nigeria.  

Pamoja na kuwa Nigeria ni nchi yenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika, raia wa nchi hiyo tayari wanakabiliwa na mfumuko wa bei wa karibu asilimia 20, uhaba wa mafuta wa mara kwa mara na usambazaji dhaifu wa huduma ya umeme katika gridi ya taifa. Majenereta yamekuwa yakitumika kwa ajili ya kusambaza umeme huko Nigeria, na wakati mwingine wananchi hulazimika kusalia bila umeme kwa muda mrefu kutokana na kushindwa kumudu gharama za jenereta.