Misri yatuma maombi ya kujiunga na kundi la BRICS
Balozi wa Russia nchini Misri amesema kuwa Cairo imetuma maombi rasmi ya kuwa mwanachama katika kundi la BRICS.
Mwanadiplomasia huyo wa Russia ameliambia shirika la habari la TASS kuwa, Misri inataka kujiunga na BRICS kwa kuwa jumuiya hiyo hivi sasa inapambana kuhakikisha kuwa miamala ya kibiashara baina ya nchi wanachama inafanyika kwa kutumia safaru za mataifa hayo, badala ya sarafu ya dola ya Marekani.
Kwa mujibu wa Balozi wa Russia mjini Cairo, Misri ina hamu ya kuimarisha ushirikiano wake wa kibiashara na Moscow. Amesema, "Mifumo mipya ya malipo kwa ajili ya mabadilishano ya kibiashara inaundwa."
Kundi la BRICS linajumuisha nchi zinazoibukia kiuchumi duniani, yaani Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini, ambazo zinaunda takriban nusu ya watu wote duniani.
Mbali na Misri na Iran, nchi nyingine mbazo zimeonesha hamu ya kujiunga na BRICS ni pamoja na Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Cuba, Comoro, Argentina, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Venezuela na Gabon.
Hivi karibuni, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa kundi la BRICS na nchi zenye azma ya kujiunga na kundi hilo walikutana huko Cape Town, Afrika Kusini. Kundi hilo ambalo lilianzishwa mwaka 2009 linajumuisha zaidi ya asilimia 41 ya idadi ya watu wote duniani na zaidi ya asilimia 28 ya pato la dunia.
Wakuu wa BRICS wamekuwa wakisisitizia udharura wa kuangaliwa upya mfumo wa utawala duniani pamoja na haja ya nchi huru kujitenga na nchi za Magharibi zinazotumia mabavu dhidi ya mataifa mengine.