Rais wa Nigeria amsimamisha kazi mkuu wa kupambana na ufisadi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i98828-rais_wa_nigeria_amsimamisha_kazi_mkuu_wa_kupambana_na_ufisadi
Rais Bola Tinubu wa Nigeria amemsimamisha kazi Mkuu wa Kamisheni ya Kupambana na Ufisadi ya nchi hiyo ambaye alikuwa akichunguzwa kwa tuhuma za kutumia vibaya madaraka. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya serikali ya Nigeria.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 16, 2023 02:29 UTC
  • Rais wa Nigeria amsimamisha kazi mkuu wa kupambana na ufisadi

Rais Bola Tinubu wa Nigeria amemsimamisha kazi Mkuu wa Kamisheni ya Kupambana na Ufisadi ya nchi hiyo ambaye alikuwa akichunguzwa kwa tuhuma za kutumia vibaya madaraka. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya serikali ya Nigeria.

Abdul Rasheed Bawa aliyekuwa Mkuu wa Kamisheni ya Kupambana na Uhalifu wa Kifedha na Kiuchumi ya Nigeria (EFCC) ni afisa wa pili wa serikali kusimamishwa kazi na Rais Bola Tinubu wa Nigeria tangu aingie maarakani Mei 29 mwaka huu akiahidi kufanya mageuzi ya kiuchumi.

Rais Bola Tinubu wa Nigeria 

Bwana Bawa ametakiwa kukabidhi haraka majukumu ya ofisi hiyo kwa Mkurugenzi wa Oparesheni wa Kamisheni hiyo ambaye atakaimu usimamizi wa kazi zote za kamisheni hiyo hadi hapo uchunguzi utakapokamilika. Abdu Rasheed Bawa anachunguzwa kwa makosa ya kutakatisha fedha, ubadhirifu na uhalifu mwingine wa kifedha, ikiwa ni pamoja na udanganyifu wa mtandaoni.

Taarifa iliyotolewa na serikali ya Nigeria imeongeza kuwa, Abdul Rasheed Bawa amesimamishwa kazi na Rais Tinubu kutokana na tuhuma kubwa zinazomkabili za kutumia vibaya madaraka. Bawa amesimamishwa kazi wiki moja tangu Godwin Emefiele aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya nchi hiyo alipofukuzwa kakzi na kutiwa mbaroni. 

Rais mstaafu wa Nigeria, Muhammadu Buhari, alifanya "vita dhidi ya ufisadi" kuwa mojawapo ya vivutio vyake wakati wa kampeni za uchaguzi wa 2015 na 2019. Hata hivyo Nigeria imeendelea kuwa miongoni mwa nchi fisadi sana duniani. Hii ni kwa mujibu wa Taasisi ya Transparency International.