Takriban watu 150 wafariki dunia baada ya boti kuzama nchini Nigeria
Takriban watu 150 wamepoteza maisha baada ya mashua waliyokuwa wamepanda kupinduka katika jimbo la Kwara, magharibi mwa Nigeria.
Vyombo vya habari vimeripoti kuwa takriban watu 150 wamefariki dunia baada ya mashua waliyokuwa wamepanda kupinduka katika jimbo la Kwara, magharibi mwa Nigeria.
Imeripotiwa kuwa wengi wa waliokuwa humo walizama na kufa maji katika eneo la Patigi kutokana na mashua hiyo kubeba watu kupita kiasi. Watu 144 waliripotiwa kuaga dunia mara tu baada ya mashua hiyo kuripotiwa kuzama, lakini idadi zaidi ya wahanga iliripotiwa baada ya tukio hilo.
Kwa mujibu wa polisi ya jimbo la Kwara, kulikuwa na watu 250 kwenye boti hiyo iliyozama, ambapo vikosi vya uokoaji na ufikishaji misaada ya dharura jana Ijumaa vilipata mabaki ya mashua hiyo iliyozama kwa msaada wa wakazi wa eneo la Patigi.
Hapo awali, idadi ya wahanga waliokufa katika tukio hilo ilitangazwa kuwa 106.
Ajali za mashua na boti za abiria huripotiwa mara kwa mara nchini Nigeria na katika nchi nyingine za Afrika hasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutokana na mashua hizo kuwa kuukuu na kubeba abiria kupita idadi inayoruhusiwa.