Wanavijiji nchini Mali washambuliana na kuuana
Serikali ya Mali imetangaza kuwa, wakazi wa vijiji viwili katikati ya nchi hiyo wameshambuliana vikali na kusababisha watu wengi kuuawa na kujeruhiwa.
Kwa mujibu wa serikali ya Bamako, mapigano hayo yamejiri kati ya wakazi wa vijiji vya Mouya na Koussouma, vilivyoko wilaya ya Mopti, katikati ya nchi hiyo ambapo habari za awali zinaeleza kuwa, jumla ya watu 14 wameuawa na wengine 40 kujeruhiwa. Kufuatia hali hiyo serikali imetuma idadi kubwa ya askari kwenda eneo hilo kwa ajili ya kurejesha hali ya usalama. Hata hivyo serikali imemtuhumu kiongozi wa mji wa Mopti kutokana na kuchelewa kuchukua hatua za dharura kuzuia mauaji hayo ya kinyama baina ya wakazi wa vijiji hivyo. Mapigano kama hayo baina ya wakazi wa vijiji hivyo ambao wamekuwa wakigombania ardhi, yaliwahi kujiri pia miaka kadhaa iliyopita. Ni vyema kuashiria kuwa, maeneo ya kaskazini mwa Mali yamekuwa yakikumbwa na mizozo ya mapinduzi ya kijeshi ambayo inachochewa na watu wenye silaha.