Feb 07, 2024 02:22 UTC
  • Umoja wa Mataifa walaani njama za kuichafua UNRWA

Maripota wa Umoja wa Mataifa wametangaza kuwa, wanalaani vikali jaribio lolote la kuharamisha na kulichafua Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).

Taarifa ya maripota wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na kusitishwa misaada ya kifedha ya baadhi ya nchi kwa shirika la UNRWA imesema: Nchi hizo zimechukua uamuzi huo baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kufikia "uamuzi wa kimantiki" kuhusiana na mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza. "Tunasikitishwa sana na uamuzi mbaya wa hivi majuzi wa karibu nchi 18 wa kusitisha msaada wao wa kifedha kwa UNRWA", imesema taarifa hiyo na kusisitiza kuwa: "Habari kwamba Israel inapanga kuifukuza UNRWA kutoka Gaza ni ya kutisha."

Philippe Lazzarini, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) amesema, Israel bado haijatoa ushahidi wowote wa madai kwamba wafanyakazi kadhaa wa UNRWA waliohusika katika Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa Oktoba 7 mwaka jana.

Awali, Yisrael Katz Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Israel alitoa mwito wa kujiuzulu Lazzarini, akikariri tuhuma kwamba wafanyakazi kadhaa wa UNRWA walishiriki katika shambulio la wapigania uhuru wa Palestina dhidi ya Israel, tarehe 7 Oktoba.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel naye amewahi kudai kuwa, umewadia wakati sasa shirika la UNRWA lihitimishe shughuli zake huko Gaza. Wamagharibi wakiongozwa na Marekani ambayo ndio muungaji mkono mkuu wa utawala wa Kizayuni wametoa kila aina ya misaada ya kisiasa na kijeshi kwa Tel Aviv tangu operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa ya tarehe 7 Oktoba na mashambulizi makubwa na yasiyo na mithili ya utawala huo dhidi ya Ukanda wa Gaza. Ukweli wa mambo ni kuwa, himaya na uungaji mkono huo umekuwa kichocheo kwa Wazayuni cha kuendeleza mashambulizi yaliyosababisha mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza.

Kuhusiana na hilo, Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Euro-Mediterania lilitangaza katika ripoti yake ya hivi karibuni kwamba, zaidi ya watu 35,000 waliuawa shahidi kutokana na uvamizi unaoendelea kufanywa na utawala ghasibu wa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Filihali na katika hatua mpya ya kuiunga mkono Israel, nchi za Magharibi, kwa kisingizio cha uongo na kutumia tuhuma za Tel Aviv dhidi ya UNRWA kama hoja, zimesitisha msaada wa kifedha kwa shirika hili la Umoja wa Mataifa, ambalo lina jukumu muhimu na la msingi katika kutoa misaada kwa watu wanaokandamizwa wa Gaza. Kusitishwa kwa misaada hii kumeongeza hatari ya kusimamisha shughuli za kibinadamu za mashirika ya Umoja wa Mataifa huko Gaza na hivyo kuzidi kuzorota hali ya mambo.

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, mashinikizo dhidi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) yanalenga kulipiza kisasi Israel cha faili la mauaji ya halaiki dhidi yake katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ). Muhammad Kanji, mwandishi wa habari wa Uturuki, anaamini kwamba, kwa kuishinikiza UNRWA, kimsingi Israel ni kweli kabisa inataka kulipiza kisasi kutokana na mchakato huo wa wazi wa mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza na kesi dhidi ya Tel Aviv iliyowasilishwa na Afrika Kusini katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).

Siku moja tu baada ya kutangazwa maamuzi ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki na ili kupunguza na kufifiza ushawishi wa hilo duniani, Israel ilianzisha propaganda ya kushambulia na kuharibu sura na haiba ya shirika la UNRWA.

Watoto ndio wahanga wakuu wa hujuma na mashambulio ya jeshi la Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza

Katika kipindi cha majuma mawili yaliyopita, habari ya kindumakuwili kuhusu UNRWA imekuwa ikitangazwa sana katika vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni na nchi za Magharibi. Habari hii ambayo inakuzwa na Wazayuni, inadai kuwa, wafanyakazi kadhaa wa UNRWA walihusika katika operesheni ya Kimbunga cha al-Aqswa Oktoba 7 mwaka jana (2023). Habari hii inawalenga wafanyakazi 12 wa shirika la UNRWA ambao ni wakazi wa Palestina wa Ukanda wa Gaza. Katika hali ambayo, ukweli wa habari hii bado haujathibitishwa, Marekani, Uingereza, Ujerumani, Italia, Uholanzi, Uswisi, Japan, Kanada, Ufaransa na Australia zimetoa radiamali kali ya habari hii na kudai kwamba, zinasimamisha misaada yao ya kila mwaka kwa shirika la UNRWA kwa sababu ya ukiukaji uliofanywa na shirika hilo la Umoja wa Mataifa. Kupitishwa kwa uamuzi huo sanjari na kutaathiri maisha ya Wapalestina milioni 2 katika Ukanda wa Gaza, ambao kwa sasa wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, maji na dawa, kutakwaza pia usaidizi wa UNRWA kwa wakimbizi milioni 5.9 wa Kipalestina katika nchi za Mashariki ya Kati kama Syria na Lebanon.

Kadhalika, hatua hii ya Wamagharibi imefanyika huku nchi zinazoiwekea vikwazo UNRWA zikiwa hazijaonyesha kuguswa na mauaji ya wafanyakazi 152 wa shirika hili lenye uhusiano na Umoja wa Mataifa tangu Oktoba 7 katika mashambulizi ya Israel huko Gaza.

Wapalestina wapatao 28,000 wameuawa shahidi tangu Israel ianzishe mashambulio ya kinyama dhidi ya Ukanda wa Gaza

Hata hivyo hatua hiyo mbali na kukabiliwa na radiamali hasi ya Umoja wa Mataifa, imepokewa kwa upinzani mkali pia wa baadhi ya nchi na taasisi za Ulaya. Norway na Ireland zimetangaza kwamba hazitafuata mkumbo wa kuiwekea vikwazo UNRWA na kusema kwamba, zitaendelea na misaada yao kwa shirika hilo. Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya sambamba na kutangaza uungaji mkono wake kwa UNRWA amesema, shirika hilo ndio mshipa wa uhai wa mamilioni ya Wapalestina wanaokabiliwa na njaa na kuenea kwa maradhi. Borrel ameongeza kuwa: "Lazima kufanyike uchunguzi huru wa madai yaliyotolewa dhidi ya UNRWA, lakini kusimamisha ufadhili wa shirika hilo kunamaanisha kutoa "adhabu ya pamoja."

Hata hivyo inaonekana kampeni na propaganda za madola ya Magharibi dhidi ya UNRWA bado zinaendelea. Hapana shaka kuwa, kusitishwa kwa msaada kwa UNRWA hasa katika kipindi hiki ambapo kuna ulazima wa kupelekwa msaada wa haraka kwa watu milioni mbili wa Gaza ambao wanakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu kutokana na vita na mzingiro wa utawala wa Kizayuni kunaweza kuibua maafa ya kibinadamu huko Gaza na kuifanya hali ya mambo kuwa mbaya zaidi ya ilivyo hivi sasa.

Tags