Maripota wa Umoja wa Mataifa walaani njama za kuichafua UNRWA
(last modified Mon, 05 Feb 2024 15:43:48 GMT )
Feb 05, 2024 15:43 UTC
  • Maripota wa Umoja wa Mataifa walaani njama za kuichafua UNRWA

Maripota wa Umoja wa Mataifa wametangaza kwamba wanalaani vikali jaribio lolote la kuharamisha na kuchafua Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).

Taarifa iliyotolewa na maripota wa UN kuhusiana na kusitishwa misaada ya kifedha ya baadhi ya nchi kwa shirika la UNRWA imesema: Nchi hizo zimechukua uamuzi huo baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kufikia "uamuzi wa kimantiki" kuhusiana na mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza. "Tunasikitishwa sana na uamuzi mbaya wa hivi majuzi wa karibu nchi 18 wa kusitisha msaada wao wa kifedha kwa UNRWA", imesema taarifa hiyo na kusisitiza kuwa: "Habari kwamba Israel inapanga kuifukuza UNRWA kutoka Gaza ni ya kutisha."

Wakati huo huo, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), Philippe Lazzarini amesema kwamba Israel bado haijatoa ushahidi wowote wa madai kwamba wafanyakazi kadhaa wa UNRWA waliohusika katika Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa Oktoba 7 mwaka jana.

Lazzarini pia amesema kuwa uamuzi wa nchi hizo wa kusimamisha msaada wa kifedha wa UNRWA ulichukuliwa kwa kukurupuka na haukuwa na mantiki.

Philippe Lazzarini

Hapo awali, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel alitoa wito wa kujiuzulu Lazzarini, akikariri tuhuma kwamba wafanyakazi kadhaa wa UNRWA walishiriki katika shambulio la wapigania uhuru wa Palestina dhidi ya Israel, tarehe 7 Oktoba.

Majuzi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema msaada wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) unapaswa kudumishwa na kusema: UNRWA ndio uti wa mgongo wa juhudi za kibinadamu huko Gaza.

Baadhi ya nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zimekata misaada yao kwa shirika hilo la UN kutokana na madai yasiyo na msingi yaliyotolewa na utawala katili wa Israel.