Hizbullah; urithi wa kudumu wa Sayyid Hassan Nasrallah
Hamjambo na karibuni kuwa nasi katika kipindi chetu cha Makala ya Wiki ambacho kinachunguza shambulizi na mauaji ya kigaidi ya Israel dhidi ya Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullah...
Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon aliuawa shahidi kikatili baada ya miaka mingi ya Jihadi na Muqawama dhidi ya Wazayuni maghasibu. Sayyid na mwana Jihadi huyo mkubwa alipigana katika safu ya muqawama kwa zaidi ya miongo mitatu, na jina lake lilikuwa likiwatetemesha Wazayuni maghasibu waliozivamia na kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina. Muhtasari wa wasifu wa Sayyid Hassan Nasrullah aliyekuwa na umri wa miaka 64 unaonyesha kuwa, Sayyid wa Mashahidi wa Muqawama alitumia karibu miaka hamsini ya maisha yake adhimu katika kuongoza mapambano dhidi ya adui Mzayuni. Baada ya kuuliwa shahidi Sayyid Abbas Mousavi, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Hizbullah hapo mwaka 1992 yaani muongo mmoja baada ya kukaliwa kwa mabavu Lebabon na kuasisiwa harakati ya Hizbullah, Sayyid Nasrullah alichaguliwa kuwa kiongozi wa Hizbullah akichukua nafasi ya Sayyid Abbas Mousavi. Sayyid Abbas Mousavi aliuliwa shahidi akiwa bado kijana mwenye umri wa miaka. Sayyid Hassan alishika hatamu za kuiongoza Hizbullah akiwa na umri wa miaka 32; na ni katika umri huo ambapo aliiongoza Hizbullah katika maswala mbalimbali na akaibadili kuwa harakati ya mapambano ya kitaifa huko Lebanon, na kuifaya taasisi bora ya mapambano na ya kisiasa yenye ushawishi ndani ya serikali na katika bunge la Lebanon. Kushindwa kwa Israel katika mashambulizi ya majira ya kiangazi 2006 ni mojawapo ya matukio muhimu ya kipindi cha uongozi wa Sayyid Hassan Nasrullah. Jeshi la Israel mbalo liliwasili Beirut ndani ya saa chache tu liliondoka kwa madhila kusini mwa Lebanon baada ya kushindwa katika vita vya siku 33.
Mbali na uongozi wa harakati ya Hizbullah, Sayyid Nasrullah alikuwa kamanda katika maidani ya vita ya Mhimili wa Muqawama na kiungo kikuu cha nguzo za mhimili huo kuanzia Gaza hadi Sana'a. Sauti na sura ya Sayyid Nasrullah ulimfanya kuwa nembo na alama ya Muqawama wa Kiislamu duniani na mapambano ya Jihadi. Alikuwa kiongozi wa harakati ambayo iliasisiwa kutokana na mapambano ya wananchi walio wengi dhidi ya watu waovu. Harakati iliwathibitishia wananchi wa Lebanon kwamba silaha ya mapambano vinaweza kuwalinda dhidi ya uvamizi wa Israel. Mafanikio ya Muqawama wa Kiislamu katika kalibu ya harakati ya Hizbullah ya Lebanon kuanzia mwaka 1985, ambayo yaliwafungisha virago Wazayuni na kuwafukuza kusini mwa Lebanon, hadi kukombolewa nchi hiyo mwaka 2000 na kushindwa Israel katika vita vya mwaka 2006, yalikuwa na nafasi ya pekee kwa Muqawama na Katibu Mkuu wake katika nyoyo za mamilioni ya watu. Nasrullah aliibuka kutoka tabaka la watu maskini wa viunga vya Beirut na kubeba silaha kwa shabaha ya kuwakomboa, wao na ardhi yao. Alimtoa mwanawe mhanga katika njia ya Mwenyezi Mungu na Muqawama wa Kiislamu na alitekeleza kwa uaminifu ahadi zake hadi dakika ya mwisho ya uhai wake. Kuuawa kwake shahidi, wakati watu wake wakikabiliwa na mashambulizi makali ya mabomu, kumepandisha juu hadhi ya Nasrullah na kufungua ukurasa mpya huko Lebanon na katika eneo la Magharibi mwa Asia.
Kuuliwa shahidi Sayyid Hassan kumewaathiri na kuwahuzunisha sana Waislamu wote na wapigania ukombozi katika pembe mbalimbali duniani. Hayati Sayyid Nasrullah alikuwa na nafasi ya kipekee katika nyoyo za wafuasi wa makundi na dini mbalimbali nchini Lebanon. Alikuwa kama baba na kaka wa wote ambaye jina na sauti yake ilikuwa faraja kwao. Weledi na busara zake vilimfanya kuwa mmoja wa watu wanaoheshimika zaidi ulimwenguni. Katikati mwa mji wa Beirut familia zilizolazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi huko Dhahiya zimemtaja Nasrullah kama shahidi ambaye amesabilia maisha yake katika kukabiliana na Israel. Nivin mkazi wa kitongoji cha Dhahiya huko Beirut ameiambia televisheni ya al Jazeera kuwa "natamani kusikia tena sauti yake. Nasrullah alikuwa kama kaka au baba kwetu na hakuwa mwanasiasa tu. Tutaendeleza mapambano ili kuifutilia mbali Israel, jambo ambalo lilikuwa matarajio yake ya siku zote."
Hassan mwenye umri wa miaka 25 anasema: "Tutaendeleza mapambano na harakati za Sayyid Nasrullah. Wananchi watakufa shahidi lakini Hizbullah itaendelea kuwepo siku zote."
Matamshi haya ya watu walioguswa na mauaji ya kigaidi yaliyofanywa na Israel dhidi ya Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sayyid Hassan Narullah yamesadikishwa pia na ripota wa televisheni ya CNN ya Marekani ambaye amesema kwamba, mauaji hayo hayawezi kusambaratisha harakati ya Hizbullah. Huku ikiashiria "nafasi muhimu" ya Hizbullah katika eneo la Magharibi mwa Asia na "uwezo wake wa juu wa silaha na upelelezi", CNN imesisitiza kwamba, "ingawa Israel inakuona kuuawa kwa Sayyid Hassan kama mafanikio, lakini ukweli ni kwamba, mauaji hayo hayatasababisha dosari yoyote katika harakati hiyo. Israel inapaswa kujifunza kutokana na historia na kutambua kwamba vitendo kama vile ugaidi havijawahi kufanikiwa katika kuharibu makundi ya upinzani."
Mwishoni mwa ripoti hiyo ya uchambuzi, CNN imeeleza kuwa: "Hizbullah imekuwepo kwa miongo minne. Hivyo haiwezekani kudaiwa kwamba muqawama wa Hizbullah umetoweka baada ya Nasrallah. Kwa sababu historia imeonyesha kwamba watateua viongozi wengine na kujipanga upya kwa ajili ya kuendeleza mapambano yao ya muda mrefu dhidi ya Israel."
Naam, damu ya kinara wa Mhimili wa Muqawama itandelea kutokota katika mishipa ya wanamapambano dhidi ya utawala wa katili wa Israel.