Gaza; Jahannamu ya waandishi wa habari
Hamjambo wasikilizaji wapendwa na karibuni kufuatilia kipindi chetu cha Makala ya Wiki ambacho kinabeba anwani: Gaza, Jahanamu ya Waandishi wa Habari”.
"Ukanda wa Gaza ni makaburi ya maelfu ya watoto." Hii ni sentensi inayotumiwa na Umoja wa Mataifa kuelezea hali ya watoto wa Ukanda wa Gaza. Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya ya Palestina, zaidi ya watoto 17,000 wa Gaza wamepoteza mzazi mmoja au wote wawili. Vilevile katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, watoto wa Kipalestina zaidi ya 16, 756 wameuawa shahidi, na 710 kati yao walikuwa watoto wachanga. Watoto 1,793 walikuwa na umri wa kuanzia mwaka mmoja hadi mitatu. Asilimia 25 ya mashahidi ni watoto wenye umri kuanzia miaka 6 hadi 12. Miongoni mwa watoto waliouawa shahidi katika Ukanda wa Gaza, kundi la umri wa miaka 6 hadi 12 ndilo linaloongoza likifuatiwa na vijana wenye umri wa miaka 13 hadi 17 ambao wengi waliuliwa shahidi na jeshi za Israel mwaka uliopita. Zaidi ya familia 902 za Kipalestina zimeuawa shahidi kikamilifu huko Gaza, na angalau familia 1,364 za Wapalestina zimebakia na ndugu mmoja tu.
Hospitali na vituo vya afya ni miongoni mwa shabaha zilizolengwa na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kisingizio kwamba, chini ya hospitali na vituo hivyo vya matibabu kuna njia za harakati ya Hamas. Mashambulizi ya Israel dhidi ya vituo hivyo afya katika mwaka mmoja uliopita yameuwa shahidi wafanyakazi zaidi ya 986 wa huduma za tiba. Utawala wa Kizayuni umezishambulia hospitali za Ukanda wa Gaza mara 90 na kuzilenga hospitali hospitali 23 kati ya 36 za eneo hilo.
Vyombo vya habari viliteseka sana katika vita vya mauaji ya kimbari vya Israel katika mwaka mmoja uliopita. Utawala wa Kizayuni ulitekeleza zaidi ya mashambulizi 1600 dhidi ya waandishi wa habari na kuua zaidi ya wana habari 175. Maripota 32 waliuawa shahidi walipokuwa wakitayarisha ripoti wakiwa wamevalia vizibao vya kuzuia risasi. Katika mwaka mmoja, zaidi ya waandishi habari 124 pia wametiwa nguvuni. Mbali na idadi hii, wafanyakazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) pia waliuawa shahidi na utawala wa Kizayuni. Haya yote ni licha ya kwamba, kwa mujibu wa kipengee cha 5 cha kifungu 50 cha Hati ya Sheria za Kimataifa, waandishi wa habari wanaotumwa katika maeneo yenye vita na mizozo wakiwajibika kwa mujibu wa taaluma yao, wanapasa kupewa ulinzi.
Mpendwa msikilizaji, hizo ni baadhi tu ya takwimu kuhusu kiwango cha kutisha cha jinai zilizofanywa na Wazayuni huko Gaza katika kipindi cha mwaka mmoja. Mwaka mmoja umepita tangu Israel ianzishe mauaji ya kimbari na mashambulizi ya kikatili dhidi ya watu wa Gaza, na kipindi chote hicho waandishi wa habari ambao wenyewe ni sehemu ya wahanga wa vita hivyo vya kinyama, wamekuwa sauti ya watu wa Palestina kwa kufichua jinai za Wazayuni maghasibu.
Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari imesema katika ripoti yake ya hivi majuzi katika kumbukumbu ya mwaka mmoja wa vita vya Gaza kwamba, mwaka uliopita ulikuwa kipindi cha mauaji makubwa zaidi ya waandishi wa habari tangu 1992, wakati ufuatiliaji wa vyombo vya habari ulipoanza kusajili nyaraka. Baadhi ya nukta zilizotolewa katika ripoti ya Kamati ya Kuwalinda Waandishi wa Habari zinasema: Waandishi wa habari 175 wameuawa shahidi katika mashambulizi ya kinyama ya Israel Ukanda wa Gaza katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Takriban wanahabari 32 waliuawa shahidi walipokuwa wakitayarisha ripoti wakiwa wamevalia vizibao maalumu vyenye nembo ya waandishi wa habari. Waandishi wengi wa habari walioko Gaza wamejeruhiwa au kupata ulemavu kutokana na kupoteza moja ya viungo vyao vya mwili. Waandishi wa habari 514 pia wamepoteza mwanafamilia mmoja au zaidi kutokana na mashambulizi ya Israel. Wakati huo huo, waandishi wa habari 124 walitiwa mbaroni na utawala wa Kizayuni, na hakuna habari zozote kuhusu hatima ya baadhi yao. Vilevile kuna wasiwasi mkubwa kuhusu kuuawa shahidi waandishi hao.
Karibu waandishi wote wa habari wanaofanya kazi Gaza mwaka mmoja uliopita wamelazimika kuhama makazi yao mara kadhaa na kuwa wakimbizi.
Waandishi wa habari ambao wameendelea na kazi zao licha ya kuwa katika mazingira magumu mara nyingi wamekuwa wakilengwa na kampeni za propaganda chafu za Israel. Katika matukio mengi, waandishi wa habari ambao wanaripoti jinai zinazofanywa na Wazayuni wametuhumiwa kuwa walihusika katika oparesheni ya Hamas ya Oktoba 7 mwaka jana ya Kimbunga cha al Aqsa, na Isral inahalalisha mashambulizi dhidi ya wafanyakazi hawa wa sekta ya habari kwa kutumia madai hayo ya uongo.
Mashambulizi na hujuma za makusudi dhidi ya waandishi wa habari na raia zinahesabiwa kuwa ni jinai za kivita kwa mujibu wa ya sheria za kimataifa. Ripoti hiyo inamnukuu Jonathan Dagger, Mkuu wa Idara ya Mashariki ya Kati ya Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka akisema: Wanajeshi wa Israel wanawauwa waandishi habari mmoja baada ya mwingine kwa mashambulizi makubwa ya anga bila ya kizuizi chochote na kauli zao zinaonyesha dharau na kukiukwa waziwazi sheria za kimataifa za masuala ya kibinadamu.
Televisheni ya al Jazeera ya Qatar Novemba 9 mwaka jana ilichapisha ripoti chini ya anwani: "Vita vya Israel na Gaza ni kwa Kiasi Gani ni Hatari Kwa Waandishi wa Habari? Ripoti hiyo ilichunguza idadi ya waandishi wa habari waliouawa katika Ukanda wa Gaza hadi tarehe hiyo. Al Jazeera ilieleza kwamba, idadi ya waandishi wa habari waliouawa katika vita kati ya Russia na Ukraine kufikia tarehe hiyo kuwa ni 17. Dadi ya waandishi wa habari waliouawa katika vita virefu zaidi vya karne ya ishirini, yaani Vita vya Vietnam, n watu 63.
Mnamo Januari 7 mwaka huu, yaani miezi mitatu baada ya kutekelezwa Operesheni Kimbunga cha al-Aqsa, televisheni ya Euronews ilitoa ripoti iliyopdewa anwani: "Idadi ya Waandishi wa Habari Waliouawa katika vita vya Gaza yazidi Jumla ya Waandishi Wote wa Habari Waliouawa katika Vita vya Pili vya Dunia" na kuripoti kuwa, waandishi wa habari wasiopungua 107 waliuawa katika muda huo. Katika ripoti hiyo, Kamati ya Kuwalinda Waandishi wa Habari (CPJ) imeeleza kuwa, waandishi habafi 69 tu waliuawa katika Vita vya Pili vya Dunia vilivyoendelea kwa takriban miaka 6, ambavyo vilikuwa vita vya umwagaji damu mkubwa zaidi duniani, ambapo mamilioni ya watu walipoteza maisha.
Israel haiwashambulia waandishi wa habari tu, bali utawala huo bandia unazishambulia pia ofisi za vyombo vya habari huko Gaza. Israel ilishambulia na kubomoa idadi kadhaa ya majengo ya maghorofa katika Ukanda wa Gaza mwanzoni mwa vita na mauaji yake ya kimbari katika eneo hilo ambapo aghalabu ya vyombo vya habari vilikuwa na ofisi zao.
Kutokana na haya yote, mashirika 60 ya habari na ya kutetea haki za binadamu yanaituhumu Israeli kuwa inafanya "mauaji ya umati dhidi ya waandishi wa habari" katika vita. Taasisi hizo zimeomba Umoja wa Ulaya kusitisha makubaliano ya ushirikiano na Israel na kuweka vikwazo dhidi ya utawala huo.
|
|