Ripoti: Watu milioni 35 ni wakimbizi Afrika sababu ya mizozo
Ripoti ya waangalizi wa kimataifa iliyotolewa jana Jumanne imesema kwamba mizozo, machafuko na majanga kote barani Afrika yameongeza mara tatu idadi ya watu waliolazimika kuyakimbia makazi yao barani humo.
Kulingana na ripoti ya shirika linalofuatilia mienendo ya watu kulazimika kuyahama makazi yao ndani ya nchi zao, IDMC, kufikia mwisho wa mwaka uliopita, bara la Afrika lilikuwa na watu milioni 35 wanaoishi nje ya makazi yao katika nchi zao.
Mkuu wa shirika hilo, Alexandra Bilak amesema kuwa, idadi hiyo ni karibu nusu ya idadi jumla ya watu waliolazimika kuyakimbia makazi yao ulimwenguni kote. Wengi wao, au watu milioni 32.5, wamekimbia vurugu na migogoro ya silaha katika maeneo yao.
Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ethiopia, Nigeria na Somalia - zinawapa hifadhi 80% ya wakimbizi na walioyahama makazi yao.
Lakini nchi hizi zote pia zinakabiliwa na majanga ambayo yanasukuma watu kukimbia yao. Mara nyingi, haya ni mafuriko: "Haya ni majanga ya ghafla na makubwa. Ingawa ukame ni majanga yanayoenea kwa muda, hivyo ni vigumu zaidi kuhesabu idadi ya watu waliohama kutokana na ukame," amebainisha Alexandra Bilak.